STAA wa Ufaransa na Real Madrid, Kylian Mbappe anaweza kukosa mechi zilizosalia za michuano ya Euro 2024, baada ya kufanyiwa upasuaji wa pua utakaomweka nje kwa zaidi ya siku 10.

Mbappe alivunjika pua katika mchezo wa hatua ya makundi wa michuano ya Euro 2024 dhidi ya Austria baada ya kugongana na beki Kevin Danso dakika ya 90, alishindwa kuendelea na kukimbizwa Hospitalini.

Daktari wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa Fabrice Bryand aliliambia gazeti la L’Equipe kwamba staa huyo anaweza kukaa nje kwa siku 10 hali ambayo itamfanya kukosa mechi zote za hatua ya makundi na kama Ufaransa haitofuzu kwenda hatua inayofuata, basi huo ndio utakuwa mwisho wake katika michuano ya mwaka huu.

Muda mchache baada ya kusambaa picha zilizomuonyesha anatoka nje ya uwanja huku akuvuja damu puani, Shirikisho la mpira wa miguu la Ufaransa, lilithibitisha kwamba ni kweli Mbappe alivunjika pua na amefanyiwa upasuaji.

Hakuna taarifa kamili juu ya wapi upasuaji huo ulifanyika lakini taarifa zinadai kuwa ni katika hospitali ya University Hospital of Düsseldorf.

Kocha wa Ufaransa Didier Deschamps alipoulizwa juu ya hali ya staa huyu alisema: "Bado haendelei vizuri, inabidi tusubiri tuone itakuwaje, siwezi kutoa jibu linaloeleweka kwa sasa, bado yupo chini ya uangalizi wa timu ya madaktari, pua yake imevunjika vibaya"

Katika mchezo huu Ufaransa iliibuka na ushindi wa bao 1-0, lililopatikana baada ya beki Maximilian Wober kujifunga dakika ya 38.

Mbali ya mechi hii, jana Jumatatu Juni 17, kulikuwa na mechi nyingine za Euro 2024, ambapo Romania ilicheza na Ukraine iliyokubali kichapo cha mabao 3-0 huku Ubelgiji ikipoteza mbele ya Slovakia kwa bao 1-0.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement