Kuelekea michezo ya Olimpiki itakayoanza kutimua vumbi Julai mwaka huu wa 2024 Paris Nchini Ufaransa, polisi mjini Paris wameanza Operesheni maalumu ya kuondoa kundi la vijana kutoka Afrika Magharibi wanaoishi kwenye mahema barabarani.

Katika operesheni hii ya hivi punde kabla ya Michezo ya Olimpiki, waliwafurusha wahamiaji hao kutoka kambi yao ya muda iliyo umbali wa hatua chache tu kutoka Mto Seine.


Operesheni hiyo imekuja siku chache baada ya polisi kutekeleza kwa kiasi kikubwa kufurusha katika kambi kubwa zaidi ya maskwota nchini Ufaransa katika kitongoji kimoja kusini mwa Paris.

Mamlaka za Nchini Ufaransa zimeeleza kuwa wanataka kuwa na mahali safi kwa Michezo ya Olimpiki hivyo hawataki watalii kuona Paris kama jiji lililojaa wahamiaji na wanaotafuta hifadhi. 

Wakati watuwakiendelea kuondoka katika maeneo hayo yasiyoruhusiwa kwa kipindi hiki, polisi wa Paris wamesema operesheni hiyo ilifanywa kwa sababu za usalama, haswa kwa sababu kambi ya hema ilikuwa karibu na shule.

Wengi wametazamia hali hiyo kama sehemu ya kujiimarisha kiusalama kuelekea michuano hiyo ya Olimpiki kutokana na wasiwasi wa usalama ambao umeongezeka kufuatia vitisho vya kundi la Islamic state (IS).

Mashindano ya Olimpiki yanatarajiwa kuanza Julai 26 hadi Agosti 11 mwaka huu huku Michezo ya Olimpiki ya Walemavu ikifuata kuanzia Agosti 28 hadi Septemba 8 mwaka 2024.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement