KUELEKEA KARIAKOO DERBY JUMAPILI, MAGETI KUFUNGULIWA SAA NNE KAMILI ASUBUHI / BODI YA LIGI YAAHIDI MAZINGIRA RAFIKI YA KIUSALAMA KWA MASHABIKI
Bodi ya Ligi nchini (TPLB) imeweka wazi juu ya maandalizi, kuelekea mchezo wa Watani wa jadi Simba SC dhidi ya Yanga SC maarufu kama Kariakoo Derby, utakayopigwa Jumapili ya Novemba 05, Uwanja wa Mkapa jiji Dar es salaam.
Afisa Habari wa Bodi ya Ligi, Karim Boimanda ameeleza kuwa, kuelekea mchezo huo Mageti yatafunguliwa majira ya saa nne kamili Asubuhi.
"Mageti ya Uwanja wa Mkapa kwa siku ya Jumapili yatafunguliwa saa nne kamili Asubuhi, na hii itatoa fursa kwa shabiki ambaye tayari anatiketi yake kuweza kuingia mapema, nba hawezi kuwa mpweke kwani kutakuwa na burudani mbalimbali na hata huduma za kibinaadam kama chakula vyote vitakuwepo, " Boimanda
Kwa upande wa suala la Usalama kuelekea mchezo huo, Boimanda ameweka wazi kuwa, kutakuwa na magari ya Doria ambayo yatazunguka eneo la Uwanja kuhakikisha kila raia anakuwa salama kabla, wakati na baada ya mchezo.
"Tumezungumza na vyombo vya usalama, kutakuwa na magari maalumu ya Doria kuzunguka Uwanja wa Taifa kwaajili ya kulinda usalama wa shabiki na mali zake, baadhi ya mashabiki wamekuwa waoga kuja uwanjani wakihofia usalama wa mali zao, niwahakikishie kutakuwa na usalama asilimia mia moja kabla na baada ya mchezo, " Boimanda.
Boimanda ameweka wazi kuwa, kwa upande wa Klabu zitapewa ulinzi maalumu ili kuweza kuondoa shida zote za barabarani.
"Klabu zote mbili yaani Simba na Yanga zitapewa ulinzi maalumu wa pikipiki kwaajili ya kuwaongoza Barabarani na hii itasaidia kuondoa shida zozote za barabarani lakini katika kambi zao, kutakuwa na maafisa usalama ambao kazi yao kuwa ni kulinda usalama wa timu, " Boimanda.