Kocha wa Chelsea Mauricio Pochettino ameondoka katika klabu hiyo kwa makubaliano baada ya msimu mmoja ndani ya Stamford Bridge.

Pochettino alichukua mikoba ya Chelsea tarehe Julai Mosi, na kusaini mkataba wa miaka miwili na chaguo la miezi 12 zaidi.

Muargentina huyo alikuwa chini ya shinikizo baada ya kufanya vibaya katika kipindi cha kwanza cha msimu lakini mfululizo wa ushindi mara tano mfululizo ili kumaliza msimu ulihakikisha kwamba anamaliza katika nafasi ya sita kwenye Ligi.

"Kwa niaba ya kila mtu katika Chelsea, tungependa kutoa shukrani zetu kwa Mauricio kwa huduma yake msimu huu," ilisema Taarifa ya wakurugenzi wa michezo Laurence Stewart na Paul Winstanley na kuongeza kuwa "Atakaribishwa tena Stamford Bridge wakati wowote na tunamtakia kila la kheri katika maisha yake ya baadaye ya ukufunzi."

Ingawa Chelsea walianza msimu vibaya na kujikuta wakiwa mkiani mwa msimamo, licha ya kutumia pesa nyingi kuliko klabu yoyote barani Ulaya, Pochettino alifanikiwa kuiongoza klabu hiyo ya London hadi nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Uingereza.

Uvumi ulikuwa umeenea kwamba kocha huyo wa zamani wa Paris St Germain na Tottenham Hotspur angeondoka baada ya mwaka mmoja tu kufundisha, lakini Pochettino alibakia kutozungumza kuhusu mustakabali wake alipoulizwa baada ya mechi yao ya mwisho ya msimu mwishoni mwa juma lililopita.

Chelsea sasa watatafuta mrithi na wameonyesha nia ya hivi majuzi kuwanunua meneja wa Ipswich Kieran McKenna, Ruben Amorim wa Sporting na Vincent Kompany wa Burnley.

Pochettino alikuwa meneja wa sita wa kudumu wa Chelsea katika kipindi cha miaka mitano, baada ya kutimuliwa kwa Thomas Tuchel na Graham Potter, ambayo ilisababisha Frank Lampard kuchukua jukumu la muda mwishoni mwa msimu wa 2022-23.

Makocha Jesus Perez, Miguel d’Agostino, Toni Jimenez na Sebastiano Pochettino pia wameondoka.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement