Kocha Mkuu wa Chelsea, Enzo Maresca ameripotiwa kumpata mchezaji mwenye uwezo wa kuja kuchukua mikoba ya Conor Gallagher.

Bado kuna utata wa kutosha juu ya hatima ya kiungo Gallagher, ambaye hana muda mrefu ataingia kwenye mwaka wake wa mwisho wa mkataba wake huko Stamford Bridge.

Kiungo huyo Mwingereza aliyeanzishwa kwenye mechi zote isipokuwa moja tu kwenye kikosi cha Chelsea katika mikikimikiki ya Ligi Kuu England kwa msimu wa 2023-24, ambapo alifunga mara tatu na kuasisti saba, ikiwa takwimu tamu kabisa alipokuwa chini ya kocha Mauricio Pochettino.

Hata hivyo, hatima ya maisha yake kwenye kikosi hicho ipo kwenye mashaka makubwa kutokana na Chelsea kupiga hesabu za kumuuza mchezaji huyo ili kuweka sawa vitabu vyao vya hesabu kwenda sawa na kanuni za Ligi Kuu England juu ya mapato na matumizi.

Tottenham Hotspur na Aston Villa zote zimeonyesha dhamira kubwa ya kunasa saini ya kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24 na zimeripotiwa kuwa kwenye mazungumzo kwa ajili ya kunasa jumla huduma yake.

Kinaelezwa kuhusu Gallagher ni kwamba anachotaka ni kuendelea kubaki Chelsea, lakini kinachoonekana ataachana na timu hiyo kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi na hilo likifanyika basi kocha Maresca atavamia kwenye klabu yake ya zamani ya Leicester City, kwenda kunasa huduma ya kiungo wao matata kabisa Kiernan Dewsbury-Hall.

Ripoti zinadai Maresca anahitaji huduma ya kiungo huyo mwenye umri wa miaka 25, akiamini ni mtu anayefaa kwenda kurithi buti za Gallagher huko Stamford Bridge. Lakini, tatizo linalodaiwa ni kwamba miamba hiyo ya King Power haipo tayari kuachana na kiungo wao Dewsbury-Hall, labda kama tu kutawekwa mezani mkwanja unaoanzia Pauni 40 milioni.

Hata hivyo, hali ya kifedha ya Leicester City inaweza kuwalazimisha kumuuza Chelsea kwa bei ndogo. Chelsea itakuwa chini ya Maresca msimu ujao baada ya kuachana na Mauricio Pochettino mwishoni mwa msimu.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement