KMC KUJIPIMA NGUVU NA AL HILAL YA SUDAN
Kikosi cha Al Hilal ya Sudan kinachonolewa na kocha maarufu Afrika, Florent Ibenge kipo nchini Tanzania na kesho jioni kitacheza mechi ya kirafiki na KMC katika uwanja wa Baobab kuanzia saa 8:00 mchana.
Mchezo huo utakuwa wa ndani ukiwa unalenga kujifunza na kubadilishana ujuzi kwa pande zote mbili huku pia wakifanya mazoezi ya pamoja ikiwa ni maandalizi ya mechi ijayo ya Ligi dhidi ya Kagera Sugar kwa KMC, huku kwa Hilal ikiwa ni maandalizi ya mechi ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Petro de Luanda, Novemba 25.
Kocha Mkuu wa KMC, Abdihamid Moallin amesema "mechi hiyo ni ya mazoezi na wataitumia kujua mapungufu na ubora wa kikosi chake kabla ya ligi kuendelea, Ligi kwa sasa imesimama, tumeendelea maandalizi kwani kwaajili ya mechi zijazo. Tulihitaji mechi za kirafiki na kwa bahati nzuri tumeipata Hilal moja ya timu bora Afrika na tutashirikiana nao," alisema Moallin na kuongeza; "Pamoja na yote tutacheza mechi ya kirafiki itakayotupa tathimini ya kikosi chetu kabla ya kuendelea na ligi tutakapocheza na Kagera."
KMC ipo nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi baada ya mechi tisa ikivuna pointi 15, na mchezo ujao itacheza ugenini Kaitaba Bukoba, dhidi ya Kagera Sugar iliyo nafasi ya nane na alama 12. Mechi itapigwa Novemba 22, 2023.