KLABU YA YANGA YATINGA NUSU FAINALI KOMBE LA SHIRIKISHO FA
BAADA ya kukosekana katika michezo saba katika mashindano tofauti sawa na dakika 630, kiungo Pacome Zouzoua amecheza dakika 20 wakati Yanga ikitinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) kwa kuichapa mabao 3-0 Tabora United kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Pacome ambaye alipata majeraha katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam, Machi 17, alikosa michezo miwili ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns nyumbani na ugenini.
Pia alikosa mechi ya FA dhidi ya Dodoma Jiji na michezo minne ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Singida Fountain Gate, Simba, JKT Tanzania na Coastal Union ambayo Yanga haikupoteza.
Fundi huyo mwenye mabao saba katika ligi aliingia katika mchezo huo dakika ya 70 wakati Yanga ikiwa mbele kwa mabao 2-0 ambayo yalifungwa na Stephane Aziz KI dakika ya 35 na Kennedy Musonda dakika ya 65.
Pacome aliomba kwa kocha wa Yanga, Miguel Gamondi kuanza kutumika taratibu tangu mchezo wa dabi dhidi ya Simba ambao Wananchi waliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Lakini Gamondi hakuwa na haraka ya kumtumia nyota huyo ambaye ni kati ya wachezaji hatari kwenye kikosi chake ambacho kina nafasi ya kutetea mataji mawili msimu huu, Ligi kuu na FA.
Coastal Union imetinga nusu fainali baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Geita Gold na inasubiri mshindi kati ya Azam na Namungo, Ijumaa Mei 3 katika Uwanja waAzam Complex, Chamazi