KLABU YA YANGA YASHIKILIA NAFASI YA MWISHO KUNDI D
Klabu ya Yanga imeshikiliwa katika sare ya 1-1 dhidi ya Medeama ya Ghana, lakini makosa ya uamuzi yaliinyima bao ambalo lingetosha kuipa ushindi wa kwanza katika mechi yao ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Baba Yara, wenyeji walitangulia kupata bao dakika ya 27 kwa mkwaju wa penalti kupitia kwa Jonathan Sowah baada ya beki wa Yanga, Dickson Job kumfanyia madhambi, Derrick Fordjour eneo la hatari.
Yanga ilijibu mapigo na kusawazisha bao hilo kupitia kwa nyota wa kikosi hicho, Pacome Zouzoua akichomoa dakika ya 36 likiwa ni la pili kwake katika mashindano haya baada ya kufunga pia mechi iliyopita dhidi ya Al Ahly katika sare ya 1-1.
Wananchi walidhani wamepata bao la pili baada ya Nickson Kibabage kuutumbukiza mpira wavuni, lakini waamuzi wakalikataa kwamba aliotea wakati picha za marudio zilionyesha hakuwa ameotea.
Katika mechi nyingine ya kundi hilo, CR Belouizdad iliiwashikilia mabingwa mara 11 wa Afrika, Al Ahly kwa suluhu mjini Cairo na kulifanya kundi D kuwa na nafasi kwa kila mmoja, Ahly wakiongoza kwa pointi 5 wakifuatiwa na Medeama na Belouizdad zenye pointi nne kila moja na Yanga imebaki mkiani na pointi mbili.
Mara ya mwisho Yanga na Medeama kukutana nchini Ghana ilikuwa ni Julai 26, 2016 kwenye Kombe la Shirikisho Barani Afrika hatua ya makundi ambapo wenyeji Medeama walishinda mabao 3-1, yaliyofungwa na Daniel Amoah huku Abbas Mohammed akifunga mawili.
Kwa upande wa bao la Yanga la kufutia machozi lilifungwa na aliyekuwa nyota wa kikosi hicho, Simon Msuva na kuifanya Yanga kuburuza mkia katika kundi lake la 'A' ikiwa na pointi nne huku Medeama ikimaliza ya tatu na pointi zake nane.
Katika msimu huo TP Mazembe ya DR Congo iliongoza kundi hilo na pointi 13 ikifuatiwa na Mo Bejaia ya Algeria iliyomaliza ya pili na pointi nane.
Baada ya mchezo huu, timu hizi zitakutana Desemba 20 katika raundi ya nne ya kundi hilo itakayochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.