KLABU YA YANGA IMEANZA MAZUNGUMZO NA MABEKI WAZAWA WA TIMU HIYO
Uhaba wa mabeki wazawa wenye uwezo wa juu, uzoefu pamoja na kutokuwa tayari kuwanufaisha wapinzani iwapo wawili hao wataondoka, ni sababu tatu za msingi zilizofanya uongozi wa Yanga kuanza mazungumzo ya haraka na mabeki wake Bakari Mwamnyeto na Kibwana Shomari kwa ajili ya kuwashawishi waongeze mikataba licha ya uwepo wa wachezaji wa nafasi nyingine ambao mikataba yao inaelekea ukingoni.
Mikataba ya Mwamnyeto anayecheza nafasi ya beki wa kati na Kibwana anayecheza beki ya pembeni, itamalizika mwishoni mwa msimu huu na kila mmoja kwa sasa yuko huru kufanya mazungumzo na kusaini mikataba ya awali ya timu nyingine kwa mujibu wa kanuni.
Ukiondoa Mwamnyeto na Kibwana, wachezaji wengine wa Yanga ambao mikataba yao itafikia tamati mwishoni mwa msimu huu ni Denis Nkane, Farid Musa, Joyce Lomalisa na Skudu Makudubela.
Hata hivyo bado mazungumzo baina ya Yanga na Nkane pamoja na Faird bado hayajaanza tofauti na Kibwana na Mwamnyeto ambao uongozi wa timu hiyo umelazimika kufanyanhivyo haraka ili kuzuia wasijiunge na timu nyingine kutokana na ubora wao.
"Miongoni mwa timu ambazo zinawahitaji wachezaji hawa ni washindani wetu kwenye mbio za ubingwa sasa ukiruhusu waondoke maana yake, mpinzani wako ananufaika kwa kuimarika huku wewe ukipunguza ubora katika kikosi chako na uwezekano wa kupata aliye bora zaidi yao ukiwa ni finyu.
"Nkane na Farid hakuna presha kubwa juu yao kwa vile nafasi wanazocheza tuna machaguo mengi lakini kwenye ukuta ni muhimu sana kupalinda," alisema mmoja wa viongozi wa Yanga.