Real Madrid imenyakuwa ubingwa wa La Liga 2023/2024 baada ya kuichapa Cadiz mabao 3-0, mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu, leo.

Huu unakuwa ubingwa wa 36 wa Ligi Kuu kwa timu hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1902.

Mabao ya kipindi cha pili ya Brahim Diaz, Jude Bellingham na Joselu yalitosha kuipa ushindi Los Blancos ya kocha Carlo Ancelotti na hivyo kufikisha pointi 87, ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote kwenye ligi hiyo msimu huu.



Madrid imetangaza ubingwa huo huku ikiwa bado ina mechi nne mkononi.

Hili ni taji la pili kwa Madrid kulichukua msimu huu baada ya kunyakuwa Spanish Super Cup kwa kuifunga Barcelona mabao 4-1 katika mchezo wa fainali.

Mbali ta mataji hayo mawili ambayo imeyapata hadi sasa Madrid pia ipo kwenye nafasi nzuri ya kupata taji la tatu msimu huu ikiwa itapenya kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kushinda.

Madrid itamenyana na Bayern Munich kwenye mchezo wa marudiano wa hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya huko Bernabeu.

Madrid inakuwa imechukua La Liga mara mbili katika kipindi cha misimu mitatu baada ya kuchukua mwaka juzi kisha ikalipoteza kwa wapinzani wao Barcelona mwaka jana kabla ya kulirudisha kwenye mikono yao mwaka huu.

Kwenye mchezo huo ulioipa ubingwa lango la Madrid lilikuwa likilindwa na kipa wao, Thibaut Courtous ambaye ulikuwa ndio mchezo wake wa kwanza wa La Liga msimu huu akirejea kutoka kwenye majeraha ya goti.









You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement