Klabu ya Rayon Sport imeingia makubaliano ya pande mbili kusitisha mkataba na mshambuliaji wake Heritier Luvumbu baada ya sintofahamu ya shangilia yake.

Luvumbu raia wa DR Congo kwenye mchezo wa Ligi dhidi ya Polisi ya nchini humo aliifungia timu yake bao la kwanza dakika ya 53, Rayon ikishinda kwa mabao 2-1 Februari 11,2024 na mshambuliaji huyo kuishangilia kwa staili ya kuhamasisha kusitishwa kwa vita ya Mashariki ya Congo.

Shangilia hiyo, ni ile anayotumia kiungo wa Yanga Maxi Nzengeli anapokuwa amefunga bao.

Mara baada ya kufunga bao hilo kisha kuishangilia kwa staili hiyo Luvumbi alijikuta kwenye wakati mgumu akikosolewa na vyombo mbalimbali vya habari kisha baadaye kuitwa Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA) mbele ya Kamati ya Nidhamu kujieleza akidaiwa kuchanganya soka na siasa.

Jana Luvumbu alikutana na uamuzi mpya mbele ya klabu yake ikimtaka kusitisha mkataba wa pande hizo mbili akielezwa uamuzi huo umetokana na presha kubwa iliyotoka nje ya klabu hiyo.

Tayari Luvumbu amerudishwa haraka nchini Congo na serikali ya nchi hiyo ikieleza inasimamia usalama wake endapo ataendelea kubaki Rwanda.

Tayari klabu yake ya zamani ya AS Vita na FC Lupopo zimeanza kumnyatia mshambuliaji huyo aliyefunga mabao 5 nchini alipokuwa Rwanda msimu huu.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement