KLABU YA MANCHESTER CITY INATAFUTA NJIA YA KUMSHAWISHI KOCHA WAO PEP GUARDIOLA KUBAKI NDANI YA TIMU HIYO
Manchester City inakuna kichwa ikipambana kuhakikisha inamshawishi kocha wake Pep Guardiola abaki Etihad baada ya mkataba wake kufika tamati mwishoni mwa msimu ujao.
Guardiola ametengeneza jina lake na kuliweka juu kabisa kama mmoja wa makocha bora kabisa kuwahi kutokea kwenye soka la dunia kufuatia mafanikio yake aliyopata akiwa na timu za Barcelona, Bayern Munich na Manchester City.
Guardiola yupo kwenye benchi la ufundi la Man City tangu majira ya kiangazi 2016. Baada ya kuwa na msimu mbaya wa kwanza, Guardiola aliibadili Man City na kuifanya kuwa timu tishio kwenye Ligi Kuu England, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Klabu Bingwa Dunia.
Chini yake, Man City imeweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kushinda ubingwa wa Ligi Kuu England kwa misimu minne mfululizo, huku akiipa pia timu hiyo mataji ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Klabu Bingwa Dunia.
Kwenye msimu uliomalizika, Man City ilifanikiwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu England, lakini ilikomea kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kuchapwa katika fainali ya Kombe la FA na mahasimu wao, Manchester United.
Guardiola ataendelea kuwamo Etihad kwa msimu wa 2024-25, lakini kitendo cha mkataba wake kubakiza miezi 12 kimeibua wasiwasi mkubwa, huku ikielezwa kwamba huenda asiendelee kubaki kwenye kikosi hicho. Bado hajaweka wazi kama ataendelea kubaki Man City au la na hilo ndilo linalowapa wasiwasi mabosi wakubwa wa Etihad.
Na sasa kumeibuka maswali ni makocha gani wanaofaa kuja kuchukua mikoba ya Guardiola atakapofungasha virago vyake na kuondoka mwishoni mwa msimu ujao.
Makocha kibao wanatajwa akiwamo wa Girona huku wengine ni Julian Nagelsmann, Roberto De Zerbi, Xabi Alonso na Mikel Arteta.