KLABU YA MANCHESTER CITY HAINA MPANGO WA KUSHUSHA BEI YA BEKI WAO JOAO CANCELO YA PAUNI 25 MILIONI
Manchester City haina mpango wa kuishushia bei Barcelona inayomtaka beki Mreno Joao Cancelo katika dirisha hili na imepanga kwenda naye katika maandalizi ya msimu ikiwa wababe hao wa Nou Camp watashindwa kulipa ada ya Pauni 25 milioni.
Cancelo (30), alicheza kwa mkopo Barcelona msimu uliopita na kiwango alichokionyesha kimeonekana kuwavutia mabosi wa timu hiyo wanaohitaji kumsajili mazima.
Hata hivyo, shida kubwa ni hali yao ya kiuchumi, na wamekuwa wakiishawishi Man City ikubali kuwapunguzia bei.
Beki huyu anajisikia furaha kuendelea kuichezea Barcelona na yupo tayari kupunguza hadi mshahara anaoupata kwa sasa ilimradi abaki, lakini changamoto ni kiasi cha pesa cha Pauni 25 milioni ambacho Man City inakihitaji kinaonekana kuwa ngumu kutolewa na Barca.
Mabosi wa Man City wamekataa kupunguza bei na wameiambaia Barca kuwa, namna pekee ya kuendelea kuipata huduma ya Cancelo ikiwa hawana pesa ya kumnunua kwa sasa ni kutoa ada ya usajili wa mkopo, kumlipa mshahara wote kwa msimu ujao na kuahidi kwamba watamsajili mazima katika dirisha la majira ya kiangazi mwakani.
Mapema wiki hii, iliripotiwa kuwa Kocha Pep Guardiola amefungua milango ya kurudi kwa beki huyo wa pembeni ikiwa ni miezi 17 tangu wawili hao waliporipotiwa wamegombana.
Pep alikaririwa akisema; “Ikiwa atauzwa ama ataenda tena kwa mkopo, ni lazima kila upande ufaidike. Timu zote mbili zikae chini zikubaliane na kama ikishindikana yeye bado ni mchezaji wetu, hivyo atarudi kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao.”
Cancelo na Pep walidaiwa kuingia katika mgogoro baada ya kocha huyo Mhispania kusema mchezaji huyo hajitumi, ndio maana hapati nafasi ya kutosha na fasta Cancelo akajibu kwa kusema kocha huyo ni muongo.
“Sijawahi kuwa mchezaji mbaya kwao, unaweza kuwauliza Nathan Ake au Rico Lewis, ndio mimi sio mchezaji bora sana wala sio mbaya sana lakini hayo ni maoni ya kocha tu.”