KLABU YA IHEFU YAREJESHA MATUMAINI LIGI KUU BARA
Klabu ya Ihefu imefufua matumaini katika Ligi Kuu Bara baada ya jioni ya leo kui-buka na ushindi wa mabao 2-1, dhidi ya Tabora United katika mchezo mkali na wa kusisimua uliopigwa kwenye Uwanja wa Highlands EstateMbarali jijini Mbeya.
Katika mchezo huo Ihefu ilipata mabao yake kupitia kwa Vedastus Mwihambi aliyefunga yote mawili dakika ya 39 na 56 huku lile la kufutia machozi kwa upande wa Tabora United likifungwa kwa kichwa na nyota wa kikosi hicho Andy Bikoko dakika ya 84. Ushindi kwa Ihefu ni kwa kwanza kwake tangu mara ya mwisho ilipoifunga Yanga mabao 2-1, Oktoba 4 mwaka huu kwenye Uwanja wa Highlands Estate kwani baada ya hapo ilicheza michezo minane ambapo kati yake ilipoteza minne na kutoka sare minne.
Matokeo hayo mabovu ndiyo yaliyoifanya timu hiyo kuvunja mkataba na aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho Mganda, Moses Basena aliyedumu kwa siku 50 tu baada ya kuteuliwa Oktoba 16 akichukua nafasi ya Zubery Katwila kisha kutimuliwa Desemba 5.
Kutokana na ushindi huo Ihefu inafikisha pointi 13 sawa na Geita Gold, Kagera Sugar na Coastal Union ila zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa hivyo kusogea kutoka nafasi ya 14 hadi 13 katika michezo 13 iliyocheza hadi sasa msimu huu. Kichapo cha Tabora ni cha tatu msimu huu katika michezo 12 iliyocheza hivyo kuiacha nafasi ya tisa baada ya kukusanya pointi 12.
Mchezo mwingine uliopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma, Mashujaa ilipokea kichapo cha mabao 2-0, dhidi ya Tanzania Prisons na kuifanya timu hiyo kufikisha jumla ya michezo minane bila ya ushindi katika Ligi Kuu Bara.
Mara ya mwisho kwa kikosi hicho kushinda ilikuwa ni ushindi wa mabao 2-0, dhidi ya Ihefu Septemba 16 hivyo kubaki nafasi ya 15 na pointi tisa katika michezo 11 iliyocheza huku Prisons ikiwa nafasi ya 10 baada ya kukusanya jumla ya pointi 14.
Mabao ya Maafande wa Prisons yalifungwa na nyota wa timu hiyo, Jumanne Elfadhili dakika ya 69 na Jeremia Juma dakika ya 90+6.