KLABU YA DORTMUND IMEFANIKIWA KUTINGA FAINALI YA LIGI YA MABINGWA ULAYA KWA KUICHAPA PSG BAO 1-0
Borrusia Dortmund imetinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuichapa Paris Saint-Germain bao 1-0 katika mchezo wa marudiano wa nusu fainali uliofanyika uwanjani Parc des Princes usiku wa Jumanne.
Mpira wa kona uliopigwa na Julian Brandt kwenye dakika ya 50 ulitua kwenye kichwa cha beki wa kati, Mats Hummels na kuutumbukiza nyavuni kufanya bao pekee lililozitofautisha timu hizo kwenye mchezo huo.
Dortmund sasa imetinga fainali kwa jumla ya mabao 2-0 baada kushinda 1-0 pia kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika uwanjani Signal Iduna Park, Jumatano iliyopita.
PSG ilifanya mashambulizi muda wote, lakini haukuwa usiku wao baada ya kugongesha mwamba zaidi ya mara moja. Matokeo hayo yanazidi kutibua rekodi za supastaa Kylian Mbappe kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na kikosi cha PSG, na huenda ikawa amecheza mechi yake ya mwisho ya michuano hiyo akiwa na jezi ya mabingwa hao wa Ligue 1 baada ya kuhusishwa na mpango wa kuachana na timu hiyo mwisho wa msimu.
Mbappe anahusishwa na mpango wa kutimkia Real Madrid, ambao usiku wa Jumatano, nayo watakuwa na kasheshe la kurudiana na Bayern Munich kwenye mchezo mwingine wa nusu fainali ya michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Los Blancos itakuwa uwanjani kwao Santiago Bernabeu kucheza na Bayern, ambao kwenye mchezo wa kwanza timu hizo zilifungana mabao 2-2.
Dortmund yenyewe itasubiri mshindi katika mchezo huo wa Bernabeu ili kujua mpinzani watakayekabiliana naye kwenye mchezo wa fainali utakaofanyika kwenye Uwanja wa Wembley, Juni Mosi.