Kazi ipo kwa beki wa Yanga, Kibwana Shomari kupenya katikati ya Joyce Lomalisa (beki wa kushoto) na Kouassi Yao (beki wa kulia) ambao kocha Miguel Gamondi anawatumia zaidi.

Kibwana ana uwezo wa kucheza beki ya kulia na kushoto, lakini kwenye mechi tisa za Ligi Kuu Bara msimu huu amecheza dakika 60 dhidi ya Ihefu akicheza dakika 57 na Coastal Union dakika tatu.

Kutokana na ushindani wa namba uliopo Yanga, mastaa wa zamani wamesema wanaamini kiwango chake hakijashuka, lakini anapaswa kuingia kwenye mahitaji ya kocha.

Aliyekuwa beki wa Simba na Yanga, Amir Maftah alisema Kibwana anatakiwa kuangalia Gamondi anahitaji kitu gani kutoka kwake wakati wa mazoezi.

"Msimu uliopita alifanya vizuri chini ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Nasreddine Nabi... nimesema kwenye mazoezi azingatie kocha anachomwambia na akifanyie kazi kwa bidii, binafsi namwamini ni beki anayejua mpira," alisema.

Kiungo wa zamani wa timu hiyo, Abdi Kassim 'Babi' alisema Kibwana ana muda wa kupambana na kumuonyesha kocha uwezo wake ili amwamini na kumpa nafasi.

"Kutoanza kikosini siyo mwisho wa safari ya kucheza kwa kiwango kizuri, dogo anapaswa kupambana zaidi ili kuisaidia Yanga" alisema.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement