Pesa siyo kila kitu. Ndicho unachoweza kusema kuhusu Tottenham Hotspur ukitazama msimamo wa Ligi Kuu England unavyosoma msimu huu. Kumbe pesa siyo kila kitu.

Baada ya mechi 10 kupigwa kwenye Ligi Kuu England hadi sasa, Spurs imeshinda nane na kutoka sare mbili, mishahara wanayolipwa mastaa wake, kidogo sana. Wanafuatia Arsenal, wao wameshinda saba na sare tatu. Nao hawajapoteza mchezo kama ilivyo kwa Spurs. Mishahara inayowalipa mastaa wake pia ni kiduchu ukilinganisha na wababe wengine, wakiwamo Manchester United na Chelsea kwenye wale vigogo wa Big Six. 

Mchezaji mwenye mshahara mkubwa kwenye kikosi cha Spurs ni Mkorea, Son Heung-min, anayelipwa Pauni 190,000 kwa wiki.

Huko Arsenal, mchezaji anayelipwa kuzidi wengine ni Kai Havertz, anayepokea Pauni 280,000 kwa wiki.

Si pesa nyingi ukilinganisha na vigogo wengine, ambapo huko Man United, mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi ni Casemiro, Pauni 350,000 kwa wiki. 

Wachezaji wanaofuatia ni Jodan Sancho, Pauni 350,000 kwa wiki, Raphael Varane, Pauni 340,000 kwa wiki na Marcus Rashford, Pauni 300,000 kwa wiki. Mastaa wote hao wanalipwa pesa nyingi kuliko vinara wa mishahara kwenye vikosi vyaSpurs na Arsenal, ambao wamekuwa moto kweli msimu huu.

Man United ipo nafasi ya nane, ikivuna pointi 15 tu katika mechi 10 ilizocheza, imeshinda tano na kuchapwa tano. Na bado wanalipa mishahara mikubwa mastaa wake.

Man City wao ambao wapo nafasi ya tatu kwenye ligi msimu huu, wakizidiwa kwa mabao ya kufunga na Arsenal, wenyewe mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa ni Kevin de Bruyne, Pauni 400,000 kwa wiki. Kwa sasa ni majeruhi.

Wanaofuatia, ambao wanalipwa mishahara mikubwa kuliko mastaa wa Spurs na Arsenal ni Erling Haaland, Pauni 375,000 kwa wiki, Bernardo Silva., Pauni 300,000 kwa wiki na Jack Grealish, Pauni 300,000 kwa wiki. 

Hata hivyo, wakali wote hao wa Man City, shughuli yao ya uwanjani kwa msimu huu ni pevu, wanalipa wanacholipwa.

Chelsea, wao mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi ni Raheem Sterling, Pauni 325,000 kwa wiki. Miamba hiyo ya Stamford Bridge, hali yao ni mbaya, wapo nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi, wakikusanya pointi 12 katika mechi l10, wakishinda tatu, sare tatu na vichapo vinne.

Kwenye kikosi cha Liverpool kinachonolewa na Jurgen Klopp, mchezaji wao anayelipwa mshahara mkubwa ni Mohamed Salah, Pauni 350,000 kwa wiki.

Miamba hiyo ya Anfield, msimu huu mambo yao si mabaya, nafasi ya nne kwenye msimamo, pointi 23 baada ya mechi 10. Wanazidiwa pointi tatu na vinara Spurs. Liverpool yenyewe imeshinda mechi saba, sare mbili na vichapo kimoja. Kwa mambo yalivyo kwenye Ligi Kuu England msimu huu timu ambazo hazina bajeti kubwa ya mishahara, ndizo zinazofanya vyema na kushika nafasi mbili za juu kwenye msimamo, zikichuana kusaka ubingwa.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement