Aliyekuwa kocha wa makipa wa timu ya soka ya Simba, Muharami Sultani (40) na wenzake, wanaendelea kusota rumande kwa siku 553 sasa, kutokana na upelelezi wa shauri lao kutokamilka.

Sultan na wenzake watano wanakabiliwa na mashtaka manane yakiwemo ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine zenye uzito wa kilo 34.89 pamoja na kutakatisha fedha.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Novemba 21, 2022 na kusomewa mashtaka yao.

Hata hivyo, tangu wafikishwe mahakamani hapo siku hiyo, hadi leo Jumatatu Mei 27, 2024, washtakiwa hao wamefikisha siku 553, sawa na mwaka mmoja na miezi sita, wakiwa rumande kutokana upelelezi wa shauri hilo kutokukamilika.

Licha ya upelelezi wa kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi namba 71/2022 kutokukamilika, pia washtakiwa hao wanaendelea kusota rumande, kutokana na mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya yanayowakabili, hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Vilevile, mashtaka ya kutakatisha fedha yanayowakabili washtakiwa hao, hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Leo, wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga aliieleza mahakama hiyo, kuwa upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea, hivyo Serikali inaomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Mwanga alitoa taarifa hiyo mbele ya hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement