ilikuwa jioni bora sana kumuona Kelvin uwanjani. Ni siku ile Tanzania inatwaa CECAFA kwa mara ya mwisho. 

Jioni ile mbele ya watoto wa Ivory Coast, mbele ya Kipre Tchete na mdogo wake Kipre Ballou, Kelvin alizima sana taa, alizima jenereta na kuondoka nalo.

Basi huyu ndiyo Kelvin aliyesimama kwenye ukuta wa taifa na jezi namba tano mgongoni kwa miaka mingi. Kwa muda alicheza Simba kisha baadae alienda Yanga Afrika. 

Lakini kamwe hakuwahi kuchuja. Kwa miaka yote Kelvin ni yuleyule.

Mgumu, mkatili, mbishi, mtemi, mkorofi. Kuna muda Yanga Afrika walimuita cotton. 

Ndani yake unatengeneza nguo, ndani yake unachuja mafuta na ndani yake unachoma Nishati. Kuna kipindi walimfananisha Vidic wa Yugoslavia.

Lakini kweli, Vidic anasema haogopi kuweka kichwa kwenye mguu kwasababu anajua jeraha likiingia mwilini linafutika lakini goli likishaingia halifutiki. 

Kazi ya beki ni kulihami lango lake. Ndiyo maana leo nimeamua kumkumbuka Kelvin. 

Huko nyuma niliwahi kuambiwa mitaa anayotokea Kanda ya ziwa ina sifa ya kuzalisha wachezaji wagumu. 

Nilibisha sana kwasababu sikuwahi kuwaona kina Kitwana Seleiman na George Masatu Magere. 

Lakini sasa nakubaliana nao kwasababu nimemuona Kelvin. 

Basi Kelvin amecheza na Erasto Nyoni wa Simba, amecheza na Cannavaro wa Pemba na baadae alimuachia usinga pale Jangwani. 

Kelvin amecheza na Aggrey Morris wa Azam na sasa anacheza na Mohamed Kassim wa Polisi. 

Bado Kelvin ni yuleyule. Yule atakayeokoa kwa mguu na kichwa. 

Yule atakayekinga tumbo lake kwenye shuti ili mpira usiingie kwenye wavu wake. 

Yule atakayemtukana beki mwenzake na kumkoromea golkipa wake ili wajipange vema. 

Bado Cotton ni yuleyule. Sasa anahesabu mwaka wa thelathini na nane na kuendelea, lakini bado kama yule wa miaka 21 pale Yaounde Cameroon.

Unakumbuka chuma mbili za Samuel Eto'o wa Barcelona zinatuondoa kufuzu world cup?? Basi Kelvin siku ile alikuwa benchi na mpaka leo anaendelea kukiwasha kwenye ligi kuu ya soka nchini Tanzania


IMEANDALIWA NA: FATUMA RASHIDI

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement