Licha ya kupoteza katika mchezo wa kwanza, michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa upande wa Wanawake, dhidi ya Mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Mamelody Sundowns kutoka Afrika Kusini, Wawakilishi wa Tanzania katika Michuano hiyo, JKT Queens wameeleza kuwa bado hawajakata tamaa kwani lengo lao lipo palepale la kutwaa Ubingwa wa Michuano hiyo inayoendeea kutimua vumbi Nchini Ivory Coast.

Mwenyekiti wa JKT Queens, Esta Ryoba ameeleza kuwa, wanaendelea kukiweka sawa kikosi ili kuendelea kuwa imara kwa kuimarisha eneo la mahitaji na kuondoa vikwazo vitakavyoikwamisha timu hiyo kutimiza malengo waliyojiwekea.

“Mahitaji yote ya wachezaji yapo vizuri, hakuna kitu ambacho kinakosekana kitakachosababisha timu ishindwe kusonga mbele, kwa hiyo kwa suala hilo na kwasababu Utawala upo vizuri kwa timu ya JKT Queens, tunaamini tunakwenda mpaka Fainali,” Ester Ryoba – Mwenyekiti JKT Queens.

Kikosi cha JKT Queens kimeendelea na mazoezi katika uwanja wa Lycee Moderne kikijiandaa na mchezo wa pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi dhidi ya mwenyeji, Athletico FC Abidjan utakaochezwa hapo kesho (Novemba 08 ) katika Uwanja wa Amadou, Karhogo.

Ikumbukwe, Katika mchezo wa awali uliopigwa Novemba 05 katika ufunguzi wa michuano hiyo, JKT Queens walipoteza kwa bao 2-0 mbele ya Mamelody Sundowns ya Afrika Kusini mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Amadou Gon Coulibaly, Karhogo nchini Ivory Coast.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement