JERAHA LA NONI MADUEKE, PIGO KWA ARSENAL
Madueke alitolewa uwanjani kipindi cha mapumziko baada ya kuonekana akichechemea mwishoni mwa kipindi cha kwanza katika sare ya 1-1 na City. Mchezaji huyo wa kimataifa wa England mwenye umri wa miaka 23 aliondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Bukayo Saka, ambaye alikuwa anarudi uwanjani baada ya kupona jeraha la msuli wa paja alilopata mwezi uliopita kwenye ushindi wa 5-0 dhidi ya Leeds.
Madueke alionekana akichechemea muda mfupi kabla ya filimbi ya mapumziko na alikuwa akitembea kwa shida alipokuwa akiwashinikiza wapinzani. Hata hivyo aliendelea kucheza na kuonekana katika maumivu makali baada ya kuzuia krosi ya mwisho wa kipindi cha kwanza kutoka kwa Jeremy Doku wa Ubelgiji.
Arsenal sasa wanafanya vipimo ili kubaini iwapo usajili wao wa majira ya kiangazi ameathirika vibaya. Tangu kujiunga na kikosi cha Emirates akitokea Stamford Bridge, Madueke ameonesha kiwango kizuri, akicheza mechi zote sita za Arsenal katika mashindano yote hadi sasa, ingawa bado hajafunga bao kwa The Gunners.
Ameanza katika michezo mitano mfululizo, baada ya kufanya debut yake rasmi kama mchezaji wa akiba kwenye ushindi wa 1-0 dhidi ya Manchester United katika uwanja wa Old Trafford. Madueke pia alianza michezo yote miwili ya timu ya taifa ya England mapema mwezi huu, akifunga bao katika ushindi wa 5-0 dhidi ya Serbia mjini Belgrade.
Baada ya mechi ya jana, Mikel Arteta alithibitisha kuwa Madueke alipata jeraha “mapema sana” kwenye mchezo huo dhidi ya City. Arsenal walipambana na kufanikiwa kupata pointi baada ya Erling Haaland kuipatia City bao la kuongoza katika uwanja wa Emirates.



