JAMIE VARDY AMEFANIKIWA KUIRUDISHA LEICESTER LIGI KUU EPL KWA KUICHAPA PRESTON MABAO 3-0
Staa wa Leicester City, Jamie Vardy juzi alifunga mabao mawili na kuipa timu yake ubingwa wa Championship wakiwa tayari wameshapanda daraja.
Leicester ilifanikiwa kuichapa Preston North End mabao 3-0 na kuchukua ubingwa huo ikiwa ni msimu mmoja tu tangu timu hiyo iliposhuka daraja kutoka Ligi Kuu England.
Vardy mwenye miaka 37, ambaye mabao yake huko nyuma yaliwahi kuipa Leicester ubingwa wa Ligi Kuu England na Kombe la FA, amefikisha mabao 20 kwenye michuano yote msimu huu.
Kasey McAteer, naye alifanikiwa kufunga bao moja na kuifanya timu hiyo ipande ikiwa sawa na Burnley, Fulham na Norwich ambazo zilikaa chini msimu mmoja tu na kupanda, zikiwa zimetwaa ubingwa.
Ushindi huo pia umeifanya Leicester kuwa klabu ya kwanza kutwaa ubingwa wa Championship mara mbili, lakini kama itashinda mechi ya mwisho itafikisha pointi 100 na kuweka rekodi nyingine ya kukusanya pointi nyingi kwa msimu.