Wakati timu chache zikiwa hazija maliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara, tayari Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi ameanza hesabu ya mechi za mzunguko wa pili, huku akiweka kikao na mastaa wake.

Yanga imeshamaliza mechi zake 15 za mzunguko wa kwanza, huku ikifikisha pointi 40 na kuwa na uhakika wakumaliza kileleni mwa msimamo kabla mzunguko wa pili wa ligi haujaanza Jumamosi ijayo.

Timu kadhaa ikiwemo wapinzani wao wa jadi Simba, bado zina mchezo mmoja mkononi.

Kocha Gamondi amekiri ligi sio rahisi, kisha akachekelea uimara wa kikosi chake akisema kabla ya kuanza mchezo wa kwanza wa mnzunguko wa pili watakuwa na mabadiliko makubwa.

Gamondi raia wa Argentina alisema kurejea kwa kikosi chao kamili baada ya kumalizika kwa Fainali za Mataifa Afrika Afcon 2023, kumeongeza morali na tayari ameshakutana nao na kuwaeleza juu ya ugumu ambao timu yao itakutana nao. Kocha huyo ambaye ameiongoza Yanga kushinda mechi 13 kati ya 15 ilizocheza za ligi alisema kila timu inayo kwenda kukutana nao inapambana kuhakikisha haipotezi kwa kipigo kikubwa hali ambayo lazima wafanye mabadiliko ya mbinu zao za kutafuta mabao.

"Tuko kamili sasa kila mchezaji yupo Aziz Ki, Djigui Diarra kina Dickson Jobwote wametimia, nafikiri hizi mechi 15 zimekuwa na changamoto mbalimbali,kuna wakati tulilazimika kucheza bila ukamilifu lakini bado tukashinda, hii nathibitisha juu ya ubora wetu,"alisema Gamondi.

"Natarajia ugumu zaidi kwenye mechi za kumalizia ligi, nimewaambia wachezaji wangu hakuna timu inayokuja kwetu ikijiandaa kupoteza, tunaona jinsi mbinu za wapinzani zilivyo kwa sasa, unaona kabisa wanadhani tutashinda nyingi ndio maana huwa hawataki kucheza na kuamua kujilinda.

"Tunaheshimu mbinu zao lakini sisi lazima tuwe na njia tofauti ya kutafuta ushindi, tutakuwa na mabadiliko machache kulingana na aina ya wapinzani tutakao kutana nao, tunatakiwa kushinda kwa kiwango bora kila timu kwenye hizi mechi zitakazofuata itakuwa na hesabu zake ili ibaki salama."

Tangu kurejea kwa ligi Yanga imeshacheza mechi nne ikishinda tatu na kutoka sare moja, ikifunga mabao matano ikiruhusu bao moja pekee na kabla ya kusimama huko kwa ligi mechi nne za nyuma ilishinda zote ikifunga mabao 11 na kuruhusu mabao mawili pekee.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement