Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma amesema hakuna kikwazo kwa Timu yoyote ya Ligi Kuu kuchagua Uwanja wa Nyumbani katika mechi zake ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akibainisha kuwa kabla ya Ligi Kuu ya Tanzania kuanza Timu zina uhuru wa kuchagua uwanja wa nyumbani utakaotumika kwenye michezo ya timu husika ndani ya Tanzania Bara au Zanzibar bila kuathiri Kanuni na miongozo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi Tanzania na Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF).

Mhe. Mwinjuma amesema hayo Novemba 8, 2023 Bungeni Jijini Dodoma kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo wakati akijibu Swali la Mhe Mussa Omar Salim (Gando) aliyeuliza Je, kwa nini baadhi ya mechi za Ligi Kuu ya Tanzania zisichezwe kwenye Viwanja vya Gombani na Amani vilivyopo Pemba na Unguja.

"Endapo timu yoyote inayoshiriki Ligi Kuu itawiwa kutumia Uwanja vya Gombani na Amani Zanzibar kama Uwanja wa nyumbani hakutakua na kikwazo chochote ikiwa timu itakidhi makubaliano na uongozi unaosimamia taratibu na matumizi ya uwanja husika bila kuathiri Kanuni na miongozo ya TFF na Bodi ya Ligi Tanzania" amesisitiza Mhe. Mwinjuma.

Ameongeza kuwa, Kanuni ya 9:7 ya Bodi ya Ligi inaruhusu timu ya Ligi Kuu kuteuwa viwanja vingine miongoni mwa Viwanja visivyotumika katika mchezo wa Ligi Kuu kwa michezo yake miwili tu ya Nyumbani na kuwasilisha uteuzi wake siku ishirini na moja kabla ya mchezo husika unaokusudiwa kuchezwa kwenye Uwanja ulioteuliwa.

Akijibu Swali la Nyongeza la Mhe. Festo Sanga kuhusu kurejesha Ligi ya Muungano, Naibu Waziri Mhe. Mwinjuma amesema tayari Wizara zinazosimamia michezo zimeshaanza utaratibu kupitia TFF na ZFF wa kurejesha ligi hiyo ambayo ni Ligi inayounganisha Watanzania na kudumisha Muungano bila kuathiri ratiba ya Ligi Kuu.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement