GEITA GOLD imefuzu Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho baada ya kuichapa Rhino Rangers mabao 2-1 katika mchezo wa raundi ya 16 bora uliofanyika Uwanja wa Nyankumbu, mjini Geita.

Na sasa Geita Gold imeungana na Namungo kwenye hatua hiyo ya Nane Bora baada ya kuichapa Kagera Sugar kwa mikwaju ya penalti 5-3 kufuatia sare ya bila kufungana katika dakika 90.

Huu ni msimu wa tatu mfululizo kwa Geita Gold kutinga hatua hiyo ya robo fainali, shukrani kwa mabao ya kipindi cha kwanza, yaliyofungwa na Jonathan Ulaya kwenye dakika ya pili na Elias Maguli, aliyefunga la ushindi dakika 20 baada ya Rhino kusawazisha kupitia Mack Samson kwenye dakika ya 10.

Katika awamu mbili zilizopita, ambazo Geita ilitinga robo fainali, ilitupwa nje na Yanga, kwa penalti 7-6 kwenye msimu wa 2020/2021 na kwa bao 1-0 msimu uliopita.

Rhino Rangers ilikuwa timu pekee isiyokuwa ya Ligi Kuu Bara iliyokuwa imesalia kwenye mikikimikiki hiyo ya Kombe la Shirikisho na sasa kikosi hicho cha First League kimetupwa nje.

Mikikimikiki hiyo ya Kombe la Shirikisho itaendelea kesho, Alhamisi kwa mchezo mmoja, ambapo Singida Fountain Gate itakipiga na Tabora United katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.





You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement