GAMONDI: YANGA HAKUNA HAJA YA DIARRA WALA AZIZ KI
Viungo washambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua,Maxi Nzengeli na Augustine Okrah kumalizana na Hausung ya Njombe katika mechi ya kiporo cha 64 Bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) itakayopigwa kesho jijini Dar es Salaam.
Yanga itaialika timu hiyo ya RCL katika mchezo huo utakaopigwa kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, huku kocha Gamondi akiweka wazi mechi hii haitawahusu wachezaji watano waliokuwa katika timu za taifa akiwapa mapumziko baada ya kurejea alfajiri ya leo kutoka Ivory Coast.
Wachezaji hao ni wanne waliokuwa na Taifa Stars, nahodha Bakar Mwamnyeto, Ibrahim Bacca, Dickson Job na Mudathir Yahya sambamba na Kennedy Musonda aliyekuwa na Zambia iliyotolewa pamoja na Tanzania katika mechi za makundi wakiwa Kundi F na kuziacha Morocco na DR Congo zikisonga mbele.
Kwa mujibu wa Gamondi anawataka wachezaji hao kambini kuanzia Jumatano mara baada ya mechi hiyo ya ASFC ambapo amesema atawatumia wachezaji wapya na wale walio kuwa hawajaitwa katika timu za taifa kumalizana na Hausung.
Mbali na nyota hao watano watakao kosekana, pia kipa Diarra Djigui na Stephane Aziz KI ambao kesho watavaana katika mechi ya 16 Bora ya Afcon wakati timu zao za taifa za Malina Burkina Faso zitakapokabiliana huko Ivory Coast, hivyo kuifanya Yanga kuwakosa nyota saba kwa mpigo katika mchezo huo wa ASFC.
Gamondi alisema anatambua umuhimu wa mchezo huo ulio mbele yao lakini anaamini wachezaji waliopo wanaweza kufanya mambo makubwa na kuivusha timu hiyo hatua inayofuata, hivyo hana presha licha ya kuwakosa nyota hao saba kesho.
"Wachezaji waliokuwa katika timu zao za taifa na wameaga mashindano wataungana na wenzao Jumatano mara baada ya mapumziko ya muda mfupi, kwa mchezo wa Jumanne natambua umuhimu wake lakini unaweza ukachezwa bila ya hao, kuna wachezaji bora kikosini ambao watabeba jukumu"alisema Gamondi na kuongeza;
"Yanga ina wachezaji wengi bora wataifanya kazi kama inavyotakiwa lengo ni kuwapa muda wachezaji anmbao wametoka kushiriki mashindano makubwa barani Afrika."
Akizungumzia maandalizi yao kwa ujumla alisema yana kwenda vizuri na wachezaji wote waliokuwa kambini wanaendelea katika hali nzuri ya ushindani anatarajia mchezo mzurikesho.
"Maandalizi yana kwenda vizuri na kila mchezaji yupo kwenye hali nzuri ya ushindani, naamini tutakuwa na mchezo mzuri Jumanne" alisema.
Wachezaji ambao watabeba jukumu lakuivusha Yanga kwenye hatua hiyo kwenda 32 Bora kuungana na timu zilizotangulia zikiwamo Namungo, Azam na Coastal Union ni pamoja na nyota wapya Augustine Okrah, Shekhan Ibrahim, Joseph Guede na wale wa zamani wakiongozwa na Paconme Zouzoua, Maxi Nzengeli, Gift Fred, Jona Mkude, Salum Abubakar, Khalid Auchona wengineo.