GAMONDI: JUKUMU NI MOJA TUU, USHINDI
Yanga kuanzia saa 10:00 jioni, itakuwa Uwanja wa Benjamin Mkapa kucheza mechi ya nne ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi dhidi ya Medeama, na mchezo wa kwanza ugenini iliilazimisha miamba hiyo ya Ghana sare ya bao 1-1, Desemba 8, mwaka huu.
Mchezo huo ni wa kufa ama kupona kwa Yanga kwani inahitaji ushindi ili kurejesha matumaini ya kumaliza nafasi nbili za juu kundi D ili kujihakikishia kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza.
Kwa sasa kundi hilo lipo wazi kwa kila timu baada ya mechi tatu likiongozwa na Al Ahly ya Misri yenye alama tano ikifuativwa na CR Belouizdad yenye pointi nne sawa na Medeama ya tatu huku Yanga ikiwa mkiani na alama mbili ilizovuna baada ya sare na Ahly nyumbani na Medeama ugenini.
Kwa maana hiyo hesabu za kwanza kwa Yanga leo ni ushindi ili ifikishe alama tano kabla ya kumalizana na Al Ahly ugenini na Belouizdad nyumbani mechi zitakazopigwa Februari, mwakani ambazo pia watatakiwa kuibuka na ushindi na kumaliza na pointi 11 zitakazowapeleka robo fainali. "Tumefanya kila kitu kuhakikisha tunapata ushindi kwenye mchezo huu mazoezini na wachezaji.
Tumeshamaliza maandalizi tunafahamu jukumu ni moja tu kuhakikisha tunapata ushindi kwa kuwa huu ni mchezo muhimu kwetu" alisema Miguel Gamondi, jana.