Yanga imerudi nchini ikitokea Ghana na mastaa wa timu hiyo leo wanarudi kambini kujiandaa na mechi mbili za ndani, huku kocha Miguel Gamondi akituliza presha kwa kuwaambia mashabiki kwamba watulie kwani hesabu bado ziko sawa.

Yanga ilikuwa Ghana kucheza mechi ya tatu ya Kundi D ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutoka sare ya 1-1 na wenyeji wao, Medeama na kuifanya ivune jumla ya pointi mbili na kuganda mkiani mwa kundi hilo, linaloongozwa na Al Ahly ya Misri na kufuatiwa na CR Belouizdad ya Algeria na Medeama yenye pointi nne.

Akizungumza mara baada ya kurejea Gamondi alisema licha ya kwamba bado hawajapata ushindi wowote katika mechi za makundi bado hawajakata tamaa kuendelea kupigania heshima na malengo ya Yanga.

Gamondi alisema bado Yanga iko ndani ya hesabu zao za kutinga robo fainali, lakini sasa wanatakiwa kuhakikisha hawafanyi makosa kwenye mechi zao tatu zilizosalia.

Yanga imebakiza mechi mbili nyumbani itakapowakaribisha Medeama Desemba 20 kisha baadaye mwakani itakutana na CR Belouzdad Februari 23 mwakani na kusafiri hadi Misri Machi 1 kumalizana na Al Ahly.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement