Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi ameshamaliza kuisoma CR Belouizdad ya Algeria wanayocheza nayo mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi Novemba 24, kwenye Uwanja wa 5 July 1962.

Alichofanya Gamondi ni kucheza na mtandao wake wa wataalam wa soka Barani Afrika. Ameinua simu moja tu kwa swahiba yake anayeishi Algeria ambaye ni mzuri kwenye kusoma mchezo na akamfanyia tathmini nzito ya timu hiyo kwa wiki kadhaa na kumpa kila kitu.

Anachofanya Gamondi kwa sasa ni kukaa na mastaa wake na kuwapa nondo za timu hiyo iliyomtimua Sven Vandebroek hivi karibuni.

Yanga imepangwa kundi hilo na timnu za Al Ahly ambao ndio mabingwa watetezi wa michuano hiyo na Medeama ya nchini Ghana iliyowahi kukutana nayo 2016 kwenye Kombe la Shirikisho Afrika na kuvuna pointi moja tu kati ya sita baina yao.

Gamondi alichogundua, moja ya silaha kubwa iliyonayo Belouizdad ni katika eneo lao la kiungo ambalo kwake sio tatizo kupambana nao kutokana na aina ya wachezaji bora wanaoweza kumudu presha hiyo. "Licha ya kuwafuatilia na kufanya tathimini ya kina juu ya wapinzani wetu, tunahitaji kujipanga katika kila maeneo kwani mchezo huo ni mgumu na sisi tunataka kupata matokeo mazuri yatakayotuweka katika nafasi nzuri mbele" alisema Gamondi.

Katika michezo mitano ya ligi ambayo Belouizdad imecheza msimu huu imeshinda mitatu na kupoteza miwili ikiwa nafasi ya nne na pointi tisa ikionekana pia sio tishio kwenye kufunga kwani kati ya hiyo imefunga

mabao manane na kuruhusu matano. Hii ina maana timu hiyo haina uwiano mzuri kwenye kufunga na kufungwa tofauti na Yanga ambao katika michezo yake tisa imeshinda minane na kupoteza mmoja huku ikiwa ni tishio kwenye kufunga kwani imefunga mabao 26 na kuruhusu matano tu.

Belouizdad juzi ilishinda bao 1-0, dhidi ya Paradou huku ikiwa na mechi nyingine ya ligi Novemba 19 dhidi ya Kabylie jambo linalowapa faida zaidi tofauti na Yanga ambayo haichezi tangu mara ya mwisho ilipoifunga Simba mabao 5-1, Novemba 5. Kwa upande wa Kocha Msaidizi wa Biashara United, Edna Lema alisema licha ya Yanga kukaa muda mrefu bila ya kucheza haitakuwa na mchezo mwepesi kwani asilimia kubwa ya nyota walioitwa timu zao za taifa ndio wanaocheza kikosi cha kwanza.

"Ni ngumu kusema moja kwa moja Yanga itaenda kuathirika kutokana na kutocheza kwa sababu kila mmoja wao anatambua sana umuhimu na ugumu uliopo na jambo jingine wachezaji wengi wameitwa timu za taifa na wanacheza hivyo sioni shida kwao," alisema kocha huyo wa zamani wa Yanga Princess.

Baada ya mchezo huo Yanga itarejea nchini kuanza maandalizi ya mchezo wa pili wa hatua hiyo wakati itakapoikaribisha Al Ahly Desemba 2, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kisha kuianza tena safari kwenda Ghana kuivaa Medeama.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement