KIUNGO aliye katika ubora wa juu, Feisal Salum, amezidi kumkaribia kinara wa mabao Stephane Aziz Ki wa Yanga baada ya kufunga bao lililoiwezesha Azam FC kupata sare ya 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons katika mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Fei alifunga bao hilo kwa njia ya penalti na kuisawazishia Azam katika dakika ya 54 baada ya beki na nahodha wa Prisons, Jumanne Elfadhil kuunawa mpira eneo la hatari na mwamuzi Ally Mnyupe wa Morogoro kuamuru adhabu hiyo.

Hilo lilikuwa ni bao la tisa kwa Fei na kumkaribia zaidi kiungo wa Yanga, Aziz Ki mwenye mabao 10 katika mbio za kuwania tuzo ya Kiatu cha Dhahabu cha ufungaji bora wa Ligi Kuu Bara.

Tangu ameanza kucheza Ligi Kuu Bara akiwa na Yanga mwaka 2018, Fei hakuwahi kufunga mabao zaidi ya sita kwenye michuano hiyo, lakini baada ya kujiunga na Azam katika uhamisho uliojaa utata hadi kuombewa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, 'aachiwe aende atakako', nyota huyo maarufu kama 'Zanzibar Finest amekuwa katika ubora wa juu kabisa mbele ya lango.



Kiwango chake kimeiwezesha Azam kuwa timu inayoongoza kwa kufunga mabao mengi zaidi katika Ligi Kuu Bara kufikia sasa raundi ya 17 ya mechi, ikiwa imepachika mabao 39 sawa na vinara Yanga ambao hata hivyo wana mechi moja mkononi kwani wamecheza mechi 16.

Hata hivyo, Azam imeruhusu mabao 13, wakati Yanga imeruhusu mabao manane tu, ikiwa timu iliyofungwa mabao machache zaidi kufikia sasa.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement