Nyota wa Azam FC, Alassane Diao na Franklin Navarro wanatarajiwa kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu.

Taarifa kutoka Azam zimesema mastraika hao wanasumbuliwa na majeraha waliyoyapata katika michezo iliyocheza ikiwamo ya kirafiki na Ligi Kuu Bara.

Mcolombia Navarro alipata jeraha la kifundo cha mguu ‘enka’ katika mchezo dhidi ya Simba uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Februari 9, 2024, baada ya kufanyiwa madhambi na beki Kennedy Juma.

Kwa upande wa Diao ambaye ni raia wa Senegal, anasumbuliwa na jeraha la goti alilolipata katika mchezo wa kirafiki na aliumia wakati akifunga bao la kichwa, aliruka juu na alitua na goti na kumsababishia maumivu.

Majeraha yake kwa vipimo vya awali vimeonyesha alipata mtulinga wa goti ‘ACT’ (Anterior cruciate Ligament) na jeraha hili hupona baada ya miezi sita hadi tisa.

Alassane na Navarro wanaungana na wachezaji wengine wanne wa Azam FC wenye majeraha makubwa ambao ni makipa Abdulai Idrissu na Ali Ahamada waliondolewa kwenye usajili wa timu kwa vile watakuwa nje muda mrefu.

Pia Malickou Ndoye pamoja na Sospeter Bajana nao wanatarajiwa kupelekwa Sauzi kwa ajili ya matibabu, hawa taarifa zao zilitolewa na klabu siku sita zilizopita.

Hata hivyo, Bajana, Malickou na Navarro wataondoka usiku wa kuamkia kesho Alhamisi kwenda Cape town na watatibiwa katika Hospitali ya Vincent Pallott, huku Diao akiendelea kutafutiwa visa na ataungana na wenzake huko.

Azam inapitia changamoto ya majeruhi kwa mastaa kwani Prince Dube, Feisal Salum ‘Feitoto’ na Gibril Sillah wanasumbuliwa na majeraha madogo madogo na hivyo kufanya jumla ya wachezaji tisa wenye majeraha kwenye timu hiyo.

Azam kesho itacheza mchezo wa Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Green Warriors kwenye Uwanja wa Azam Complex, hatua ya 32 Bora.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement