AZAM imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Yanga katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa leo usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku kiungo Feisal Salum ' Fei Toto' akifunga na kuomba msamaha.

Fei Toto aliyejiunga na Azam msimu huu akitokea Yanga, amewafunga waajiri wake wa zamani lililokuwa bao la pili na la ushindi kwa Azam dakika ya 52 ya mchezo.

Baada ya kufunga Fei Toto alishangilia kidogo, kisha kuonyesha ishara ya kuomba msamaha kwa mashabiki wa Yanga ambao wakati anaondoka alikuwa kwenye mgogoro wa kimkataba na timu hiyo.

Bao la Fei Toto limekuwa la 13 kwa msimu huu na kulingana na Stephanie Aziz Ki wa Yanga.

Ushindi huu umefuta unyonge wa Azam kwa Yanga, katika mechi sita zilizopita imeshinda mara moja tu April 25, 2021, huku ikifungwa mara nne na mara moja kutoka sare.

Azam imepanda nafasi ya pili na pointi 47 na kuizidi Simba kwa alama mbili, huku Yanga akisalia kileleni ikiwa na pointi 52 kupitia mechi 20.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement