Baada ya kutokuonekana kwa muda mrefu uwanjani kiraka wa Yanga, Farid Mussa amesisitiza ushindani ni mkubwa kikosini lakini atapambana.

Chini ya kocha Miguel Gamondi amecheza dakika 26 tu kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya KMC timu yake ikiibuka na ushindani wa mabao 5-0, hivyo amekosekana kwenye mechi nyingine nane walizocheza.

"Nilikuwa majeruhi, ila nimerudi naendelea na maandalizi kama kawaida, suala la kucheza namwachia Kocha Gamondi, mimi napambana kuhakikisha namshawishi ili aweze kunipa nafasi ya kucheza," alisema Farid ambaye aliwahi kucheza Ulaya.

"Sijakata tamaa nitapambana kuhakikisha napata nafasi ya kucheza ili kuwa miongoni mwa wachezaji ambao wameipa mafanikio timu japo sio rahisi lakini inawezekana;

"Nilikuwa nje kwa muda na timu iliendelea kufanya vizuri hivyo nina kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha napata nafasi ya kucheza kama ulivyokuwa msimu uliopita," alisema. "Mimi nacheza nafasi nyingi uwanjani lakini ukiangalia zote zina watu wazuri na wote wana mchango mkubwa kwenye timu kazi kwangu kuhakikisha napambana ili kupata nafasi," alisema.

Kocha wa zamani wa Yanga, Charles Mkwasa alisema timu ina wachezaji zaidi ya 28 ni wachezaji 11 wanaotakiwa kucheza hivyo ni Suala la mchezaji kupambana ili apate namba kikosi cha kwanza.

"Kocha anapanga kikosi kutokana na uwezo wa kila mchezaji kwenye uwanja wa mazoezi, Farid ni mchezaji mzuri na mzoefu, kazi kwake ni kupambania nafasi yake kama ilivyokuwa misimu ya nyuma tangu amejiunga na Yanga," alisema Mkwasa.

Staa wa zamani wa Tanzania Prisons, Yona Ndabila alisema, "Yanga ina ushindani mkubwa kutokana na kuwa na vipaji vingi vyenye uwezo kazi kuhakikisha  anapambana kurudisha namba kikosi cha kwanza kwani anauwezo mkubwa na kipaji cha hali ya juu," alisema.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement