Michuano ya Euro 2024 imeendelea kutimua vumbi usiku wa Jumatatu kwa michezo miwili mikubwa ya kundi B- Uhispania ambayo ilikuwa timu ya pili kufuzu kwenye hatua ya 16 bora wamecheza na Albania huku Croatia wakimenyana na Italia.

Katika mechi iliyochezwa mjini Duesseldorf, Uhispania iliifunga Albania 1-0 na kukamilisha hatua ya makundi ya Euro 2024 kwa kushikilia nafasi ya kwanza ya kundi B, baada ya kushinda mechi zote tatu na kujikusanyia jumla ya alama 9.

Bao la Uhispania lilipachikwa nyavuni na winga wa timu ya Barcelona Ferran Torres katika dakika ya 13, na hivyo kuzima shauku ya mashabiki wa Albania waliokuwa wengi uwanjani hapo. Hata hivyo, mchezo huu haukuwa rahisi kwa timu ya Uhispania ambayo ilifanya mabadiliko makubwa ya wachezaji wake ukilinganisha na mechi yao dhidi ya Italia siku nne zilizopita na ambapo walijipatia pia ushindi wa 1-0.

Ni mara ya kwanza tangu mwaka 2008 kwa Uhispania kushinda mechi zote tatu katika hatua ya makundi iwe kwenye Kombe la Dunia au michuano ya Euro. Kocha Luis de la Fuente sasa anajipanga kuelekeza nguvu zake zote kwenye mchezo wa hatua ya 16 bora utakachezwa mjini Cologne siku ya Jumapili dhidi ya mshindi wa tatu ambaye bado hajafahamika.


Italia yailazimisha Croatia sare ya 1-1

Katika mechi nyengine ya kusisimua, Italia waliilazimisha katika dakika za mwisho Croatia sare ya 1-1 baada ya bao maridadi la Mattia Zaccagni. Italia wanasonga mbele katika hatua ya mtoano ya Euro wakishikilia nafasi ya pili na itamenyana na Uswisi katika hatua ya 16 bora, huku Croatia ikiwa katika hatihati ya kuondolewa lakini bado ina matumaini ya kusonga mbele na hii itategemea na matokeo katika mechi zingine baadaye wiki hii.

Wakiwa na pointi mbili pekee uwezekano ni mdogo kwa kikosi hicho cha Zlatko Dalic kufuzu kama moja ya timu nne bora zilizo nafasi ya tatu lakini bado inawezekana.

Luka Modric ambaye ana umri wa miaka 38, na siku 289, alipachika bao hilo dhidi ya Italia katika dakika ya 55, muda mchache tu baada ya kipa wa Italia Gianluigi Donnarumma kuzuia mkwaju wa penati.

Modric sasa anashikilia rekodi ya kuwa mfungaji mwenye umri mkubwa zaidi kwenye michuano ya Euro. Awali rekodi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na Ivica Vastic, ambaye alikuwa na miaka 38, na siku 257 alipoifungia Austria dhidi ya Poland kwenye michuano ya Euro mwaka 2008.

Kufuatia matokeo ya jana, tayari England, Ufaransa na Uholanzi zimefanikiwa kufuzu katika hatua ya mtoano. Uingereza imefuzu kutoka Kundi C huku Ufaransa na Uholanzi wakisonga mbele kwenye Kundi D.

Lakini timu zote tatu zitacheza mechi zao za mwisho za hatua ya makundi siku ya Jumanne, ambapo zitajaribu kuwa miongoni mwa timu mbili bora ili kuziwezesha kukutana na timu ambazo wanadhani si tishio sana katika hatua ya 16 bora.

Michuano hiyo inaendelea hii leo, Ufaransa watashuka dimbani na Poland huku Uholanzi wakipambana na Austria. Baadaye usiku, Denmark watachuana na Serbia huku England wakimenyana na Slovania. Mtanange wa kwanza kufahamika katika hatua ya 16 bora ni kati ya Uswisi ambao watachuana na Italia Jumamosi ya Juni 29.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement