ENGLAND INAPASWA KUJIVUNIA KWA KUWA NA HUDUMA YA JUDE BELLINGHAM KWENYE KIKOSI CHA TIMU YA TAIFA
Kiungo wa Ujerumani, Toni Kroos amesema England inapaswa kutamba kutokana na kuwa na huduma ya Jude Bellingham kwenye kikosi chao, staa ambaye anaweza kuwapa nafasi ya kufanya vizuri kwenye fainali za Euro 2024 zitakazoanza Ujerumani, kesho, Ijumaa.
Kroos anamfahamu vyema kutokana na kuwa pamoja kwenye kikosi cha Real Madrid kilichobeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mapema mwezi huu, ambapo lilikuwa taji ya 15 kwa miamba hiyo ya Hispania.
Bila shaka presha kubwa itakuwa kwa kiungo kinda Bellingham kwenye kuhakikisha kikosi cha Three Lions kinafanya kweli na kunyakua taji.
Kroos alisema: “Nilipata faida ya kucheza na Jude Bellingham kwa miezi 12 iliyopita na hakika unaweza kuona kiwango chake bora akiwa kwenye umri wa miaka 20 tu. Hata akiwa nje ya uwanja, Bellingham amepevuka zaidi.
“Hakuna wachezaji wengi wa aina yake, hivyo matumaini mengi ya England yatakuwa kwake. Pale Real Madrid baada ya wiki chache tu, akageuka na kuwa mchezaji anayefanya uamuzi ndani ya uwanja.”
England ilichapwa 1-0 na Iceland kwenye mchezo wa kirafiki Ijumaa iliyopita na haina siku nyingi itatupa kete yake ya kwanza kwenye Euro 2024, ambapo Jumapili itakipiga na Serbia kwenye kipute cha Kundi C.
Bellingham hakuwa amecheza kwenye mechi hiyo ya kirafiki kwa sababu alipewa mapumziko ya siku kadhaa kwa kuwa alitoka kwenye mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyofanyika Juni 1.
Kroos alisema: “Jude Bellingham ni mtu wa nguvu na ni kifurushi kilichosheheni. Ni aina ya mchezaji ambaye anaweza kumudu presha. Najua atacheza kwa ubora wake kwa kadri anavyoweza. Naamini atakwenda kuwa mchezaji atakayeamua mambo kwenye kikosi cha England.”