NAHODHA wa JKT Tanzania, Edward Songo amesema atavaa kinyago usoni kwa wiki tatu, ili kulinda usalama wa pua, pia kuondoa hali ya hofu inayomsumbua, kutokana na tukio la kuumia uwanjani, kumrudia mara kwa mara mawazoni.

Songo aligongana na kipa wa Mashujaa, Patrick Muntari, katika mechi iliyopigwa Machi 6 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, wakati anauwahi mpira akafunge kwa kichwa, akagongana na Muntari, na kulazimika kuwahishwa Hospitali ya Muhimbili kwa ndege, ili kuokoa maisha yake.

Tayari Songo amemaliza miezi miwili nje ya uwanja, aliyoambiwa na daktari na leo ameonekana kwenye picha ya mazoezi ya timu, usoni akiwa amevaa maski anayotakiwa kudumu nayo wiki tatu.

Ameulizwa kwa nini ameivaa maski? Akajibu; "Kuna mshipa wa pua ilipasuka karibia na jicho, akili bado ina woga, daktari aliniambia itanisaidia kukaa sawa, pia kulinda pua, hivyo nimeambiwa niivae ndani ya wiki tatu."

Songo ambaye amefunga mabao manne kwenye Ligi Kuu, ameulizwa endapo kama atacheza na haya ndio majibu yake, "Kama kocha ataona nafaa kuwa kikosini nipo tayari kwa kazi."

JKT Tanzania ni mwenyeji wa Yanga katika mchezo wa kesho Aprili 23 kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, uliopo Mbweni, Dar es Salaam.






You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement