Kikosi Cha Yanga kimesharejea jijini Dar es Salaam alfajiri ya jana na moja kwa moja kwenda kambini kujiandaa na mechi ijayo ya Kundi D ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri, huku kipa tegemeo wa timu hiyo, Diarra Djigui akiwatuliza mashabiki akiwaambia wasiwe na hofu.

Yanga ilikuwa Algeria kupepetana na CR Belouizdad iliyoshinda mabao 3-0 na wikiendi hii itakuwa wenyeji wa Al Ahly iliyoanza kwa kishindo kwa kuifumua Medeama ya Ghana kwa mabao 3-0 jijini Cairo katika mechi nyingine ya kundi hilo, huku kipa Diarra aliyekosekana kwenye mchezo wa Belouizdad akisema kazi ndio imeanza na mashabiki wa klabu hiyo hawapaswi kuwa na wasiwasi kutokana na matokeo ya ugenini. Kipa huyo raia wa Mali alifunguka juu ya hali yake kwa kushindwa kudaka mechi hiyo ya kwanza, lakini akiwatoa hofu mashabiki na kuwataka kujitokeza kwa wingi kwenye mchezo ujao utakaopigwa Kwa Mkapa.

Diarra alisema anasumbuliwa na maumivu ya bega, licha ya kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Mali ambayo hata hivyo haikumtumia kwa vile ametakiwa kupata mapumziko zaidi ili kuwa kwenye hali nzuri ya kurudi uwanjani. "Naendelea vizuri na ninafanya mazoezi na wenzangu, tatizo langu la bega halikuwa kubwa ila lilihitaji kupata mapumziko ya muda mrefu kiasi ili kujiweka hali nzuri ya ushindani nafikiri muda ukifika mtaniona uwanjani" alisema Diarra na kuiongeza;

"Siwezi kuweka wazi ni lini ila nipo kwenye hali nzuri mashabiki watarajie kuniona uwanjani muda wowote nafurahia upendo wao kwangu, nimepokea meseji nyingi kutoka kwa Wanayanga na ninawahakikishia hatutawaangusha." Kuhusu mechi iliyopita, 

Diarra alisema ulikuwa ni mzuri na wenye ushindani, lakini bahati haikuwa upande wao wamesahau matokeo hayo wanajipanga kwa mchezo muhimu zaidi wa Jumamosi dhidi ya Al Ahly.

"Tumepoteza, hii ni sehemnu ya matokeo tumeumia, ila tunajipanga kwa mchezo mwingine ambao ni muhimu zaidi dhidi ya Al Ahly nyumbani hatuwezi kurudia makosa tunahitaji pointi zote tatu ili kurudi kwenye mstari na mashabiki wajiandae kupata ile burudani waliyoizoea," alisema kipa Bora huyo wa Ligi Kuu Bara kwa misimu miwili mfululizo.

Diarra alisema wataingia kwenye mchezo huo kwa kuwaheshimu wapinzani wao hao, huku wakiwa na kumbukumbu ya maumivu ya kupoteza mchezo wa kwanza kwa idadi kubwa ya mabao na kudai ndio soka lilivyo, hivyo mashabiki wasahau yaliyopita na kujitokeza kwa wingi.

"Tumepoteza, lakini sio mwisho wa michuano. Bado tuna nafasi ya kufanya vizuri nyumbani tumejifunza makosa hatuwezi kurudia, mashabiki wake kutupa nguvu," alisema.

Yanga imerejea kamili ikiwa na Rais wao, Injinia Hersi Said na Makamu, Arafat Haji walioenda kushuhudia mechi iliyopita na leo mastaa wataendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo wa Al Ahly utakaokuwa ni wa 11 baina yao katika michuano ya CAF tangu 1982. Mechi 10 zilizopita zikiwamo nane za Ligi ya Mabingwa na mbili za Shirikisho, Yanga imeshinda mara moja tu.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement