Simba inakabiliwa na kibarua kigumu cha kuhakikisha ndoto za kusaka ubingwa kwa msimu huu zinabaki hai wakati itakapokaribishwa na Coastal ambayo tangu iwe chini ya Mkenya David Ouma imeonyesha sio ya kuichukulia poa.

Kitendo cha Simba kupoteza mechi iliyopita mbele ya Tanzania Prisons kiliifanya Simba ijikute ikitengeneza pengo la pointi saba na Yanga kabla ya mechi ya jana dhidi ya Namungo, hivyo kupoteza pointi tatu au hata kutoka sare leo, kimahesabu kutazidi kufifisha matumaini yake ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.

Kwa upande wa Coastal hiyo ni mechi ya kimkakati kwake kwa vile inahitaji kupata ushindi ambao utazidi kuiweka katika mazingira mazuri ya kujihakikishia nafasi ndani ya nne za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Coastal hadi sasa inashika nafasi ya nne ikiwa imekusanya pointi 27 wakati Simba ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 36.

Wakati Simba ikiingia katika mechi hiyo huku ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Prisons kwa mabao 2-1, Coastal yenyewe imetoka kulazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Azam FC.

Ni mechi ambayo inakutanisha timu moja inayofanya vizuri zaidi katika mechi za nyumbani dhidi ya timu ambayo inatamba ugenini msimu huu.

Coastal mechi tisa ilizocheza nyumbani hadi sasa, imepata ushindi mara tano, kutoka sare mbili na kupoteza michezo miwili wakati Simba katika mechi nane ambazo imeshacheza ugenini, imepata ushindi mara saba na kutoka sare moja.

Wagosi wa Kaya wamekuwa na unyonge wa muda mrefu mbele ya Simba na pengine leo wanaweza kuvunja minyororo ya kuteswa na Simba katika Ligi Kuu kwa kupata ushindi vinginevyo wataendeleza historia ya kuonewa na Wekundu hao.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement