CAFCL: YANGA YAJIHAKIKISHIA ROBO FAINALI LIGI YA MABINGWA AFRIKA
YANGA tayari ina uhakika wa kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuifyatua CR Belouizdad ya Algeria wikiendi kwa mabao 4-0 na leo itatafuta heshima nyingine ya kutaka kuongoza Kundi B wakati itakapoikabili Al Ahly ya Misri katika mechi ya kufungia hatua ya makundi ya michuano hiyo kwa kundi hilo.
Yanga itakuwa wageni wa watetezi hao wa taji la michuano katika pambano litakalopigwa kuanzia saa 1:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki, kila timu ikitaka kumaliza kama kinara ili kukwepa ule mtego wa mechi za robo fainali katika droo itakayopangwa wiki ijayo jijini Cairo.
Al Ahly kwa sasa ndio vinara wa kundi ikiwa na pointi tisa, huku Yanga liyopo ya pili ina alama nane na matokeo ya ushindi kwa timu mojawapo itaipa nafasi ya kuongoza kundi na kusikilizia sasa timu zitakazoshika nafasi ya pili katika makundi ya A, B na C na itakayomaliza ya pili itakuwa na kibarua dhidi ya vinara wa makundi hayo matatu katika robo.
Yanga imetua jijini humo ikitambia rekodi nzuri kundini, kwani ndio timu inayoongoza kwa mabao mengi hadi sasa, lakini ikiwa ni pekee iliyoifunga bao Al Ahly katika sare ya 1-1 ya mechi iliyopigwa jijini Dar es Salaam.
Akili ya Yanga ni kuhakikisha inapata ushindi mbele ya Al Ahly, lakini wenyeji nao wakitaka kulinda heshima ya nyumbani kwa kutambua kama itaruhusu kupoteza leo itatibua rekodi tamu iliyonayo kwa timu za Tanzania kwenye ardhi ya nyumbani iliyodumu tangu mwaka 1982. Al Ahly haijawahi kupoteza mechi yoyote nyumbani mbele ya klabu za Tanzania, hivyo inajua ikizembea kidogo kwa kikosi cha Miguel Gamondi mambo yanaweza kuwaendea kombo na kung’olewa kileleni kuwapisha wapinzani wao kuongoza kundi hilo lenye Medeama ya Ghana pia.