Saa 4 usiku. Yanga itakuwa palepale iliposhinda siku ile dhidi USM Algers lakini wakakosa Kombe la Shirikisho Afrika sababu ya kikanuni tu.

Yanga ilicheza na USM Alger katika mechi ya pili ya fainali ya michuano ya msimu uliopita na kushinda bao 1-0 la mkwaju wa penalti ya Djuma Shaban. Hata hivyo ushindi huo ulifanya matokeo ya jumla kuwa 2-2, kwani tayari ilishapasuka nyumbani kwa mabao 2-1 na Waalgeria wakabeba taji mbele ya Yanga.

Sasa leo usiku, kikosi cha Yanga imerudi tena jijini Algiers tayari kuvaana na wenyeji wao, CR Belouizdad katika mechi ya kwanza ya Kundi D ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu. Kocha Miguel Gamondi amesisitiza kwamba Yanga iko tayari kukiwasha huku akionyesha kuwatisha wenyeji alipoweka wazi kwamba amefanya kazi yake ipasavyo kabla hawajakanyaga uwanjani usiku huu. Ameweka wazi kwamba alikuwa na mtaalam maalumu aliyemfanyia kazi ya kuisoma kiundani CR Belouizdad ndani na nje ya uwanja na amejiridhisha kwamba nondo zote alizompa ni sahihi na ameshazifanya kazi.

Kwa mantiki hiyo, kama hakutakuwa na mabadiliko yoyote ya ulazima ataanza na Diarra, Yao, Lomalisa, Mwamnyeto, Bacca, Aucho, Mudathir, Pacome, Musonda, Maxi na Aziz KI. Ndio maana anapata kiburi cha kuingia kwa kujiamini kwenye mchezo huo ambao Kocha wa CR Belouizdad, Mbrazili Marcos Paqueta akikiri kuhofia historia ya Yanga kwenye Uwanja unaotumiwa kwa mchezo wa leo. Awali Yanga ilishinda bao 1-0 hapo dhidi ya USM Algiers kwenye fainali ya Shirikisho msimu uliopita.

Yanga itaanza mechi hizo za hatua ya makundi ikiwa na kumbukumbu kwamba mara ya mwisho kucheza hatua kama hii ilikuwa miaka 25 iliyopita. Yanga ilicheza makundi na kuweka rekodi ya kuwa klabu ya kwanza nchini mwaka l998 baada ya CAF kurekebisha michuano hiyo kutoka Klabu Bingwa Afrika hadi kuwa Ligi ya Mabingwa mnamo 1997.

Na sasa timu hiyo inarudi ikiwa na kikosi imara ambacho msimu uliopita tu, kilishtua kwa kucheza fainali ya kwanza tangu klabu hiyo izaliwe 1935 katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika. Ilibaki hatua moja tu Yanga kuchukua taji hilo lililochukuliwa na USM Alger kikanuni. Ilikuwa Juni 3, 2023 ambapo iliwashtua mashabiki wa USM Alger na kuwafanyia vurugu zilizowagharimu baadae.

Yanga haikuwahi kukutana na Belouizdad hapo kabla ambapo timu zote mbili zitakwenda kuandika historia ya kwanza kwenye mechi hiyo kabla ya kurudiana baadaye. Katikati refa leo atakuwepo raia wa Chad, Alhadji Allaou Mahamat. Mabingwa hao wa Tanzania tayari wapo Algeria kwa siku tatu kabla ya mchezo huo wakitua kwa mafungu matatu kutokana na wachezaji wengine kuwa timu za taifa.

Ni mshambuliaji, Leone Wamba raia wa Cameroon aliyefunga hat trick wakati wanatinga makundi, Kocha wake anahofia fitinesi yake, lakini amewaomba mashabiki waje kwa wingi uwanjani kuwapa nguvu wachezaji wa timu hiyo. Mbali na Wamba anayeongoza kwa ufungaji ligi ya kwao sambamba na Boussouf Ishak wenye mabao mawili kwenye ligi, Yanga inatakiwa kuwa makini pia na Darfalou Oussama, kiungo Benguit Abdelraouf wenye bao moja kila mmoja.

Yanga itakutana na mshambuliaji Meziane Bentahar anayeivaa Yanga kwa mara ya tatu akihamia hapo akitokea USM Alger ambao walicheza na mabingwa hao wa Tanzania kwenye mechi mbili za fainali za Shirikisho Afrika msimu uliopita.

Kwenye mechi zao tano zilizopita, Yanga haijaangusha alama yoyote kwenye ligi wakiringia safu yao ya kiungo iliyopewa jina la MAP (wakimaanisha Maxi Nzengeli, Aziz KI Stephanie na Pacome Zouzoua) ambao wako kwenye moto mkali msimu huu tangu uanze. Nyota hao watatu wamefunga jumla ya mabao 18 kati ya 26 katika Ligi, Aziz na Maxi wakiwa na saba kila moja na Pacome akitupia mawili.

Yanga itahitaji ushindi au sare katika mechi hiyo ili iwe kuongeza morali kabla ya kurudi nyumbani wiki ijayo kucheza na watetezi wa taji la michuano hiyo, Al Ahly ya Misri waliopo nao kundi moja.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement