BRUNO GOMES ATANGAZA KUACHANA NA KLABU YA SINGIDA FOUNTAIN GATE
Kiungo mshambuliaji wa Singida Fountain Gate, Mbrazili Bruno Gomes ametangaza kuachana na klabu hiyo kwa makubaliano ya pande mbili.
Nyota huyo aliyeitumikia timu hiyo kwa misimu miwili akitokea klabu ya Jacobinense EC ya kwao Brazil, amethibitisha taarifa za kuondoka kwake kupitia mtandao wake wa kijamii wa Instagram.
"Leo nina habari muhimu ya kuwashirikisha. Baada ya kutafakari kwa kina na majadiliano (kati yake na klabu) tumefikia uamuzi mgumu, lakini tunaamini ni bora kwa pande zote zinazohusika," ameandika katika mtandao huo.
"Ningependa kuwajulisha kwamba kumekuwa na uvunjaji wa mkataba kwa upande mmoja kutoka kwa klabu na kwa bahati mbaya hii imesababisha kumalizika kwa uhusiano wangu na klabu. Uamuzi huu haukuwa rahisi, lakini ulifanyika kwa nia ya kuhakikisha tunaweza kuendelea mbele kwa njia ambayo ni chanya na yenye ujenzi kwa wote.
"Ingawa mkataba wetu umefikia kikomo, jua kwamba upendo na heshima niliyo nayo kwenu (mashabiki wa Singida Fountain Gate) itabaki milele. Kamwe sitasahau athari mliyonayo kuondoka kwangu kama mchezaji na kama mtu.
"Ahsante kwa kuwa name. Natumaini tutaendelea kuwa na uhusiano mzuri hata kama njia zetu zitachukua mielekeo tofauti."
Msimu uliopita ndio ambao ulikuwa bora wake ulikuwa mkubwa kwani alifunga mabao 10 katika Ligi Kuu Bara na kuzivutia timu Simba na Yanga.
Licha ya msimu huo kuwa bora, lakini mambo yamekuwa magumu kwake msimu huu kwani nyota huyo hadi anaondoka amefunga bao moja tu baada ya kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara.