Licha ya Simba kupoteza ugenini kwa bao 1-0 juzi usiku mbele ya Wydad Casablanca katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliopigwa mjini Marrakesh, Morocco wadau mbalimbali wa soka wakiwamo wachezaji wa zamani wa timu hiyo wamesifu uwezo wa kikosi hicho, huku wakiipa matumaini ya kupenya robo fainali.

Simba ilipoteza mechi hiyo ikiwa ni ya kwanza katika Kundi B, kwani michezo miwili ya awali ilitoka sare dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast na Jwaneng Galaxy ya Botswana na kuifanya ifikishe pointi mbili tu hadi sasa kundini ikiburuza mkia, lakini wadau hao walisema timu hiyo bado ina nafasi ya kuvuka kwenda robo fainali.

Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ismail Aden Rage alisema licha ya kikosi hicho kupoteza, bado anaona kina nafasi ya kufuzu hatua ya robo fainali ipo hasa kama itaendeleza kiwango ilichoonyesha juzi kwa kushinda mechi ya marudiano na Wydad kama huyo ndiye mbaya wao kwa sasa.

"Ningependa nizungumzie Simba na Yanga kwa sababu kiukweli zimeonyesha ile hofu ya kuziogopa timu za Kaskazini imeisha kwani ukiangalia jinsi zinavyocheza unaona kabisa wachezaji wanapambana japo makosa ni madogo madogo tu," alisema Rage.

Rage aliongeza matumaini ya timu zote kufuzu bado yapo, ingawa amewataka mashabiki kuacha kuzodoana bali wawe kitu kimoja kwa lengo la kutimiza malengo hayo kama ambavyo nchi nyingine zimekuwa zinafanya inapokuja suala la michuano ya CAF.

"Mechi ya juzi Simba ilibadilika sana kuanzia jinsi ya ukabaji na hata ukakamavu wa wachezaji ulikuwa ni mkubwa sana ila shida ninayoiona kwa timu zetu zote mbili ziboreshe haraka eneo la ushambuliaji kwa sababu ndiko ninapoona kuna shida."

Kwa upande wa nyota wa zamani wa timu hiyo, Boniface Pawasa alisema robo fainali ya Simba iko mikononi mwa Wydad hivyo mchezo wa marudiano ni lazima ishinde huku akiwataka kuongeza umakini zaidi katika utumiaji wa nafasi wanazozitengeneza.

"Nimpe pongezi kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha kwa sababu nimeona mabadiliko kwa muda mchache aliokuwa na timu hiyo hivyo namuona akifuzu hatua inayofuata kwani ukiangalia mwenye uhakika hadi sasa katika kundi hilo ni ASEC Mimosas tu."

Kabla ya mechi hiyo, Simba itakuwa na kazi ya kumalizana na Tembo FC katika mechi ya 64 Bora ya Kombe la Shirikisho (ASFC) kisha ile ya Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar zitakazopigwa kati ya Desemba 12 na 15 kisha ndipo itavaana na Wydad inayoshika nafasi ya tatu kwa sasa kwa pointi tatu ilizovuna kwa Mnyama, huku Asec ikiongoza kundi na pointi saba na Jwaneng inafuata nyuma ikiwa na pointi nne basda ya kila moja kucheza jumla ya mechi tatu hadi sasa.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement