Jumla ya Sh18 bilioni zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa barabara zinazokwenda katika uwanja wa mpira wa kisasa mkoani Arusha, ikiwa ni maandalizi ya michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON).

Hayo yamesemwa leo Jumanne, Mei 28,2024 Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Zainab Katimba wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Arusha Mjini Mrisho Gambo.

Gambo amesema Serikali inaenda kujenga uwanja wa mpira wa kisasa kwa gharama ya Sh286 bilioni, lakini hakuna barabara hata moja ya lami ambayo inakwenda katika uwanja.

“Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara ya lami ikiwa pamoja na barabara ya Njoro mkoani Arusha ili kuleta maana kwenye uwanja wa AFCON,”amesema.

Akijibu swali hilo, Katimba amesema Serikali inatambua umuhimu wa miundombinu mizuri ya barabara kuelekea katika uwanja huo wa AFCON.

“Serikali tayari imeshafanya utambuzi wa barabara hizo muhimu na imebaini kuwa kuna mtandao wa barabara wa jumla ya kilometa 13 ambazo zimeshafanyiwa usanifu na imebainika kuwa zitahitaji Sh18 bilioni kwa ajili ya ujenzi,”amesema.

Amemhakikishia kuwa Serikali itahakikisha Sh18 bilioni zinapatikana kwa ajili ya ujenzi barabara hizo ili ziweze kufanana na uwanja ule mzuri wa AFCON unaotaka kujengwa.

“Niwahakikishie zitajengwa barabara nzuri kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja hiki,”amesema.

Ujenzi wa uwanja huo ni sehemu ya maandalizi ya michuano ya AFCON itakayofanyika mwaka 2027 ambapo Tanzania imepata heshima ya kuwa mwenyeji wa mashindano hayo.

Machi 19 mwaka 2024, Serikali ilitiliana saini mkataba wa ujenzi wa uwanja huo utakaojulikana kwa jina la Dk Samia Suluhu Hassan na Kampuni ya China Railway Construction Engineering Group (CREG) ya Nchini China.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro alisema uwanja huo wa kisasa zaidi katika nchi za Afrika Mashariki, utakuwa na uwezo wa kuingiza watu 30,000 pamoja na vyumba vya watu mashuhuri pande zote mbili za uwanja.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement