Mabosi wa Simba inaelezwa watakuwa na kikao cha kwanza cha kinidhamu na kiungo wao, Clatous Chama leo kwa njia ya mtandao, akiwa huko huko kwao Zambia, lakini upande wa pili kuna jipya kutoka kwa kocha wake, Abdelhak Benchikha ambaye anatajwa kutafuta mbadala wa Mzambia huyo.

Benchikha hajafurahishwa na nidhamu ya Chama hata baada ya kukosea na sasa amewaambia viongozi wake, kwenye msako wa wachezaji wapya anaowataka waongeze na ishu ya kumtafuta mrithi wake.

Hivi karibuni, Simba ilitoa taarifa Chama ameondolewa klabu hapo na kupelekwa kwenye kamati ya nidhamu ya timu hiyo.

Kilichomtibua Benchikha ni kuona kama Chama alidhamiria kufanya makosa ya kinidhamu dhidi ya kocha wa viungo hasa baada ya Mzambia huyo kutoomba radhi hadi sasa, huku akionekana kuweka vijembe kwenye mitandao ya kijami. Hatua ya Chama kutoomba radhi imemfanya Benchikha awaambie mabosi wake sio rahisi kwake kuendelea na mchezaji wa namna hiyo na amewataka kusaka kiungo mpya wa juu atakayeweza kuziba nafasi yake hata kama atarudishwa kikosini.

Kwenye ujumbe wake kwa mabosi wake Benchikha ambaye ni kocha mwenye misimamo mikali ya kusimamia nidhamu alisema hataki kuwa na mchezaji ambaye atajiona yuko juu zaidi ya makocha wake waliopo, wachezaji wenzake au hata viongozi. "Kocha anasema yuko tayari kuheshimu wachezaji wake, lakini hayupo tayari kufanya kazi na mchezaji anayejiona yuko juu ya kila mtu na ameshataka atafutiwe kiungo mchezeshaji anayeweza kucheza nafasi ya Chama," alisema bosi huyo wa juu ambaye yumo kwenye kamati ya usajili wa Simba.

"Hatua ambayo imemkera kocha ni Chama kutoomba radhi hadi sasa, anaona kama alidhamiria kufanya ambacho amefanya ingawa tunaambiwa Chama na yeye ana malalamiko yake, ndiyo maana kamati itakwenda kuwasikiliza."

Mwishowe sisi viongozi tutafanya kile ambacho kocha anataka tukifanye, hili la kutafuta mtu mbadala wa Chama halina namna lazima mchakato wake uendelee kama ambavyo kocha ameagiza."

Inaelezwa Simba imekuwa ikifanya juhudi za kumpata kiungo huyo, huku ikikumbana na wakati mgumu kwa kuwa wachezaji wa daraja la juu kwenye soka kwa sasa wengi hawauzwi, Mkuu wa Kitengo cha Habari Simba, Ahmed Ally alisema kwa ufupi: "Ninachofahamu ishu ya Chama ipo kwenye kamati, hivyo tusubiri itoe taarifa."

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement