BAYERN MUNICH KUTINGA ROBO FAINALI YA LIGI YA MABINGWA ULAYA
Mabao mawili ya mshambuiliaji nyota kutoka Engand, Harry Kane yameiwezesha Bayern Munich kutinga robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, baada ya kuzima Lazio ya Italia kwa mabao 3-0 na kutinga hatua hiyo kwa jumla ya mabao 3-1.
Katika mechi ya awali ugenini, Bayern ilichapwa bao 1-0 na usiku wa jana ikiwa Uwanja wa nyumbani wa Allianz Arena, iliingia ikiwa na kazi ya kusaka ushindi ili kupoza presha kubwa aliyonayo kocha Thomas Tuchel baada ya mambo kaenda harijojo katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) ikiwa imeachwa pointi 10 na Bayer Leverkusen.
Mabao hayo mawili yamemfanya Kane kufikisha jumla ya mabao sita katika michuano hiyo akiwa na kikosi hicho kilichomsajili msimu huu kutoka Tottenham Hotspur, lakini yamemfanya afikishe 33 aliyoifungia Bayern tangu ajiunge nayo, yakiwamo 27 ya Bundesliga akiwa ndiye kinara kwa sasa. Mabao hayo sita yamemfanya alingane na Kylan Mbappe wa PSG ambaye usiku wa jana pia alifunga mabao mawili wakati timu hiyo ya Ufaransa ikiifumua Real Sociedad ya Hispania.
Bayern imeingia robo fainali ikiwa ni msimu wa tano mfululizo na ndilo taji inayoweza kulibeba msimu kama italikomaliza kwani kwenye Bundesliga mambo ni magumu na tayari imeshatema mataji mengine ya ndani huko Ujerumani.
Nayo PSG ya Ufaransa ikiwa ugenini huko Hispania ilipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Real Sociedad na kuifanya ifuzu robo kwa jumla ya mabao 4-1 kwani katika mchezo wa kwanza jijini Paris, wababe hao walishinda 2-0.