Pamoja na kumtimua Moses Basena, Ihefu inafikisha idadi ya makocha watatu hadi sasa kuachana nao ikiwa ni zaidi ya mechi walizoshinda kwenye mechi 12 ilizocheza kwenye Ligi Kuu.

Ihefu ilianza na John Simkoko aliyedumu kwa mechi mbili akimuachia kijiti Zuberi Katwila ambaye naye aliiongoza mechi nne kisha kutimkia Mtibwa Sugar na kumleta Basena raia wa Uganda aliyesimamia michezo saba. Basena katika mechi saba alizosimamia timu hiyo, amepoteza mechi tatu na sare nne na kuiacha nafasi ya 14 kwa pointi 10 baada ya michezo 12 iliyocheza kwa ujumla akiwa hajawahi kupata ushindi na timu hiyo.

Mbali na makocha, timu hiyo imeonekana kuwa mwiba mkali kwenye vyeo vingine kwani kabla ya kumtangaza Biko Scanda kuwa mtendaji mkuu, alitangulia Muhibu Kanu ambaye wameachana kimyakimya.

Basena alisema licha ya matokeo kuhusika kwenye uamuzi huo, lakini bado alikuwa na uwezo wa kuibadili timu hiyo kutokana na kikosi alichokikuta. Alisema hajahusika na usajili, lakini hata wachezaji hawana ubora kutokana na wengi kutumika kwa muda mrefu, hivyo alitarajia dirisha dogo kukisuka upya.

"Wachezaji wote nimewakuta na wengi ni kama wamechoka, mimi siyo mganga wa kienyeji japokuwa nilikuwa nasubiri dirisha dogo nifanye maboresho, lakini nakubaliana na walichoamua," alisema Basena.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement