ESPERANCE imeendeleza tena unyonge mbele ya Al Ahly baada ya kupoteza mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa uliopigwa leo katika dimba la Cairo International.

Ahly ambayo imechukua taji lao la 12 la michuano hii, ilishinda bao 1-0 ambalo lilipatikana baada ya kiungo mkabaji wa Esperance Roger Aholou kujifunga dakika ya nne.

Hii ilikuwa ni fainali ya tatu kuzikutanisha timu hizi ambapo Ahly sasa ndio inaongoza kushinda mbili na Esperance moja.


Katika kipindi cha misimu mitano Ahly imefanikiwa kuchukua taji hili mara nne, huku mbili kati ya hizo zikiwa ni msimu uliopita na huu uliomalizika.

Esperance ilikuwa inapambana kwa ajili ya kuchukua taji lao la tano na lakwanza tangu mwaka 2019 lakini ikashindikana.

Kabla ya mechi hii ya fainali kwenye misimu mitatu iliyopita Esperance imetolewa mara mbili na Ahly kwenye hatua ya nusu fainali ya michuano hii.

Mchezo wa fainali ya kwanza uliopigwa Tunisia kwenye uwanja wa Stade Hammadi Agrebi, Tunis ukahudhuriwa na mashabiki 35,000 ulimalizika kwa suluhu.


Kwa ubingwa huu Ahly imejikunjia Dola 4 milioni ambayo ni zawadi ya mshindi wa kwanza wakati Esperance ikitapata Dola 2 milioni.

Sankara William Karamoko ambaye kwa sasa anaichezea Wolfsberger AC ya Austria aliyojiunga nayo Januari mwaka huu akitokea Asec Memosa ndio ameibuka mfungaji bora wa michuano hii akimaliza na mabao manne.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement