Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz KI amesema anaiona timu hiyo ikifunga idadi kubwa ya mabao msimu huu tofauti na msimu uliopita kutokana na kutokumtegemea mchezaji mmoja.

Yanga hadi sasa ina mabao 20 kati ya hayo ni matatu tu yamefungwa na nafasi tofauti na kiungo ambayo ni bao la Dickson Job, Keneddy Musonda na Hafiz Konkoni mengine yote yamefungwa na viungo. Aziz Ki amesema kocha Miguel Gamondi ametengeneza timu ya ushirikiano na kuhakikisha inatafuta pointi tatu muhimu bila kujali nani atafunga siku hiyo.

"Yanga ina wachezaji wengi wenye uwezo wa kuona goli hivyo kila anayepata nafasi ya kucheza anaingia uwanjani akiwa na akili ya kuipambania timu kupata matokeo mazuri apambane kufunga na kuzuia hili kwa asilimia kubwa limefanikiwa; "Naweza nikakosa nafasi ya kufunga akafunga Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua, Clement Mzize, ukiangalia hadi mabeki wanafunga, hivyo kazi yao sio kulinda tu wanatakiwa kupanda kutengeneza mashambulizi pia wakipata nafasi wafunge kama ilivyo kwa Job,"

Aziz Ki amesema umoja walioutengeneza ndio siri kubwa ya kucheza kwa kujiamini na kutumia vizuri nafasi wanazozipata akikiri kuwa msimu uliopita haikuwa hivyo kwasababu walikuwa wanaamini katika kumtengenezea nafasi ya mshambuliaji tu.

Amesema Gamondi amewapa akili kubwa ambayo inawatesa wapinzani wao kila wanapokutana kwani wakimkaba yeye kwa kuamini kuwa ndiye atakayewaadhibu anafunga mchezaji mwingine ambaye hawajamtarajia.

"Hakuna raha ya kucheza mpira bila presha kutoka kwa wapinzani kama ilivyo Yanga ya sasa tunafanya kile ambacho tunaelekezwa na kocha na kimekuwa kikitulipa ubora wetu ni kutokana na kutokujipa umuhimu tunapokuwa uwanjani kila mmoja anachukuliwa kujua anachokifanya uwanjani." amesema kiungo huyo kinara wa upachikaji mabao.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement