Nahodha Msaidizi wa Simba, Mohamed Hussein amesema ushindi katika mchezo dhidi ya Azam ni muhimu kwa kikosi chao ili kipunguze pengo la pointi dhidi ya watani wao, Yanga nakuendelea kupambania ubingwa wa Ligi Kuu Bara, ushindi katika mchezo huo unaopigwa CCM Kirumba kesho hauepukiki.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo, Februari 8,2024 jijini Mwanza, Hussein amesema Azam ina kikosi kizuri na hapo ilipo haijabahatisha kuwa nafasi ya pili kwenye msimamo, hivyo Simba wataingia kwenye mchezo huo kupambana kuanzia dakika ya kwanza hadi 90.

"Tuko tayari kwa mchezo wa kesho na maandalizi yako vizuri. Mashabiki wa Simba watapata burudani kesho, jambo muhimu ni matokeo ya timu kila mchezaji anakuwa na wajibu wakupigania nafasi na kuitumikia timu kupata matokeo," amesemna Hussein.

Ameongeza kuwa: "Kwetu wachezaji hakuna mwenye presha, maandalizi yameenda vizuri kabisa kuhakikisha tunapambania pointi tatu. Kikubwa ambacho tunapambania kupata pointi tatu na kuzidi kupunguza pengo la pointi ambalo lipo (dhidi ya wapinzani wao). Kwa hiyo kila mchezo ambao upo mbele yetu ni kama fainali," amesema Hussein.

Katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, Simba inakamata nafasi ya tatu ikiwa na alama 29 huku Azam ikiwa ya pili ikikusanya pointi 31 na Yanga inaongoza.

Kwa upande wake, Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola akizungumzia maandalizi ya kikosi chake, amesema mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na ubora wa vikosi vya timu zote mbili na kusisitiza kwamba hawatawachukulia poa wapinzani wa kwani watahakikisha wanapata pointi tatu.

Matola amesema kutokana na ugumu wa ratiba wataendelea kubadilisha wachezaji na kutoa nafasi kwa kila mchezaji huku akiwatoa hofu mashabiki kuhusu kiungo Fabrice Ngoma, kwani tayari amejiunga na timu na yupo jijini Mwanza na kwamba, anaweza kuwa sehemu ya kikosi kwenye mchezo huo.

"Tunajua ubora na ugumu wa Azam tunajipanga kuhakikisha tunapata

pointi tatu. Safari ni ndefu, tulilijua hilo na tumeweza 'kumeneji wachezaji wote wako salama. Tunaamini tutakuwa tayari kwa mchezo na kufanya vizuri. Mashabiki tunataka tuwahakikishie kwamba kesho tutafanya kile kitu ambacho kila mwana Simba anakitarajia," amesema Matola

Meneja wa Habari wa Simba, Ahmed Ally amesema timu hiyo ilikuwahai ikimbii Azam, bali ratiba ilibadilika kutokana na majukumu ya kimataifa na kwamba sasa muda umefika wa kufanya jambo lao kwa kuifunga Azam.

Simba na Azam zilipangwa kucheza mchezo huo tangu mwaka jana, lakini ilishindikana kutokana na Wekundu wa Msimbazi kukabiliwa na mchezo wa makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad, kisha mashindano ya Kombe la Mapinduzi, halafu ligi ilisimama kupisha fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika ambako Taifa Stars ilikuwa ikishiriki.

"Kama tulikuwa tunawakimbia hatimaye muda umefika, Ijumaa Kirumba. Msimu uliopita Azam wamechangia kuharibu mnalengo yetu tukapoteza mbio za ubingwa wa ligi na wakatutoa kwenye Shirikisho. Kwa hiyo kesho ni siku ya Mnyama kwenda kutimiza malengo yake," ametamba za Ahmed.

"Mchezo huu ni zawadi kubwa kwa wakazi wa Mwanza na Kanda ya Ziwa. Tumewaletea burudani ya aina yake. Ni moja kati ya mechi bora kwenye ligi inapocheza Simba na Azam, imekuwa mechi ya kuvutia. Wito wangu nikwamba tunawahitaji mashabiki wote wa mpira wa miguu wakiongozwa na mashabiki wa Simba - kesho twende tukaushuhudie mchezo huu.

"Tunakiri kwamba mchezo ni mgumu kutokana na aina ya mpinzani tunayekutana naye. (Azam) wamefanya usajili mzuri na wana kikosi kizuri, lakini wanakutana na Simba ambayo gari limewaka na tunaingia kwenye mchezo huu tukiwa na chaguo moja tula ushindi. Sisi ndiyo wenyeji wa mchezo huu lazima tuungane kushawishi watu kuhudhuria mchezo huu."

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement