Ligi Kuu Bara unaendelea tena leo kwa mechi mbili zitakazopigwa viwanja viwili tofauti, huku macho na masikio yakielekezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex wakati vinara wa ligi hiyo, Azam na maafande wa JKT Tanzania zitakapovaana na kila upande ukipiga mkwara mzito moto utawaka Chamazi.

Azam na JKT zitaumana kuanzia saa 1:00 usiku, lakini mapema jioni kwenye Uwanja wa Liti itapigwa mechi nyingine kati ya Singida Fountain Gate itakayoikaribisha KMC iliyotoka kupigwa mabaio 5-0 na Wanalambalamba kwenye mchezo uliopita.

Ushindi iliyopata Azam mbele ya KMC uliifanya ikwee kileleni mwa msimamo ikifikisha pointi 25 baada ya mechi 11 iliishusha Yanga yenye pointi 24 iliyotokana na michezo tisa na iliyokuwa ikitekeleza majukumu ya mechi za kimataifa kama ilivyo kwa Simba iliyopo nafasi ya tatu na alama zao 19 ikicheza michezo minane tu.

Mchezo wa leo unatarajiwa kuwa mgumu kutokana na ukweli JKT imetoka kulazimishwa sare ya 2-2 na Singida katika mechi iliyopita iliyopshuhudiwa wenyeji wakilazimika kusawazisha bao jioni na maafande hao wakimpokeza kiungo Hassan Nassor Machezo' aliyeonyeshwa kadi nyekundu.

Rekodi zinaonyesha mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana kwenye Uwanja wa Azam Complex ilikuwa ni Oktoba 30, 2020 na kushindwa kutambiana kwa kutoka sare ya 1-1, Azam ikipata bao kupitia kwa Salum Abubakar ´Sure Boy' aliyepo Yanga kwa sasa na lile la JKT likifungwa na Michael Aidan. Huu ni mchezo wa kwanza baina ya timu hizo kukutana katika Ligi tangu JKT irejee Ligi Kuu ikitoka Ligi ya Championship.

Hii ni mechi itakuwa na kazi kwa wachezaji wa timu zote, hasa mabeki wa JKT kuwa na kazi ya kuwazuia washambuliaji wa Azam wanaoongozwa na Prince Dube, Idd Seleman Nado Kipre Junior, Gjibril Sillah na Feisal Salum ambao wameonekana kuwa moto kwa mechi nne zilizopita wakifunga jumla ya mabao 16.

Pia washambuliaji wa JKT chini ya Danny Lyanga, Sixtus Sabilo, Hassan Kapalata, Najim Magulu na Edward Songo watakuwa na kibarua cha kujipanga ili kuupita ukuta wa Azam unaoongozwa na Daniel Amoah, Charles Manyama, Cheikh Sidibe na Lusajo

Mwaikenda ambao umeruhusu bao moja tu katika mechi nne zilizopita. Kocha msaidizi wa Azam, Bruno Ferry alisema malengo yao ni kufanya vizuri huku akitoa angalizo kwa wachezaji kutobweteka, huku kwa upande wa kocha, Malale Hamsini wa JKT akisifu uwezo wa Azam ila alisema hawahofii chochote na watashuka Azam Complex kwa nia ya kupambana ili wavune pointi katika mechi hiyo, kwa lengo la kuwasaidia kadri ligi inavyoshika kasi.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement